Viongozi wa wafanyabiashara Mkoa wa Njombe wametoa wito kwa wafanyabiashara wote waliopo katika maeneo mbalimbali mkoani humo kujitokeza kupata huduma za kikodi katika Ofisi Inayotembea.
Wametoa wito huo leo tarehe 27 Aprili, 2026 ambapo, wamepongeza juhudi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kuendana na kasi ya teknolojia na kuhakikisha wanaboresha huduma ikiwemo kufikika kirahisi.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Halmashauri ya Njombe Bw. Eliudi Mgeni amesema kuwa wafanyabiashara wanapaswa kujitokeza kwani ni haki yao kupata huduma za kikodi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara kwenye Viwanda na Kilimo Bw. Menard Mlyuka amesema kuwa kulipa kodi ni wajibu wa kila Mtanzania hivyo wafanyabiashara wanapaswa kutekeleza wajibu wao wa msingi.
Viongozi hao wameipongeza serikali na uongozi wa TRA kwa kuendelea kuwa karibu na walipakodi na kurahisisha huduma.


