Na Gregory Milanzi, MTWARA
Wadau kutoka taasisi mbalimbali mkoani Mtwara wameaswa kuimarisha ushirikiano katika kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu kwa kutoa elimu kwa wananchi na kuimarisha uratibu wa hatua za kisheria na kiutendaji.
Wito huo umetolewa leo, Julai 23, 2026, na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dkt. Benedicto Ngaiza, wakati akifungua semina kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu na uhamiaji salama.
Akizungumza katika semina hiyo, Dkt. Ngaiza amesema usafirishaji haramu wa binadamu ni uhalifu mkubwa unaokiuka haki za binadamu na kudhalilisha utu wa mwanadamu.
Amesema uhalifu huo unaathiri zaidi wanawake, watoto, vijana na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi, hivyo kuna umuhimu wa wadau kushirikiana kwa karibu ili kuuzuia.
Baadhi ya washiriki wa semina hiyo wamesema mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka kwani yanagusa tatizo linaloendelea kujitokeza katika jamii, huku wananchi wengine wakijihusisha na vitendo hivyo kwa kujua au bila kujua.
Akitoa mfano wa tukio lililotokea mkoani humo, Naibu Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mtwara, Bahati Sendela, amesema vijana 30 walishawishiwa kutoka Dar es Salaam kwa ahadi ya kupata ajira Mtwara, lakini walipowasili hawakukuta kazi yoyote kama walivyoahidiwa.
Amesema mmoja wa vijana hao alimtumia ujumbe baba yake akiomba atumiwe fedha za chakula baada ya kubaini kuwa ahadi walizopewa hazikutekelezwa. Alieleza kuwa waliambiwa wagharamie safari kwa fedha zao na kwamba wangerejeshewa walipofika, jambo ambalo halikufanyika.
"Baada ya zaidi ya mwezi kupita bila kupata kazi wala kurejeshewa fedha zao, baba wa mmoja wa vijana alipiga simu na kutueleza walipo. Tulimtafuta mtu aliyewaleta na kumtaka awarudishe vijana wote 30 Dar es Salaam," amesema Sendela.
Semina hiyo imeandaliwa na Shirika la CVM kwa ufadhili wa Serikali ya Italia na Chama cha CHODAWU, kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Sekretarieti ya Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Watu (ATS).
Washiriki wa semina hiyo walitoka katika vyombo vya ulinzi na usalama, Mahakama, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Idara ya Uhamiaji, Maafisa Ustawi wa Jamii, viongozi wa dini, viongozi wa serikali pamoja na wawakilishi wa asasi za kiraia.


