Atoa Maagizo 10
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi amewata watumishi wa wizara hiyo kuzingatia mambo 10, ya msingi na kisisitiza nidhamu, haki, weledi na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu na wajibu wa wizara wa kulinda raia na mali zao.
Ametoa maagizo hayo wakati akifungua Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ambacho kimefanyika Aprili 28, jijini Dodoma ambapo kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Ally Senga Gugu, Wakuu wa Idara na Vitengo wa wizara, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Katungu, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, CGF John Masunga, Kamishna wa Fedha na Lojistiki wa Jeshi la Polisi, CP Liberatus Sabas, Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, CP Kombo Khamis Kombo, Wawakilishi wa Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na wawakilishi wa watumishi wa wizara.
“Naomba tuzingatie yafuatayo Moja, kusimamia na kuhakikisha mpango mkakati, mipango dira, dhima na majukumu ya wizara yanatekelezwa kwa ufanisi, kufikia malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, mbili, kuzingatia miongozo mbalimbali ya kisera ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.
Tatu, kuhakikisha watumishi wote wanaostahili wanapandishwa vyeo kwa wakati.” amesema Katambi.
Katika hotuba yake hiyo ya kufungua Baraza, Waziri Katambi ametaja agizo lingine la nne ni kulipa madai ya wastaafu, uhamisho, likizo, stahiki, madeni na madai ya watumishi kwa wakati kuipunguzia serikali malimbikizo ya madeni.
Tano ni kuhakikisha watumishi wa wizara wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, haki, maadili na taratibu bila kutumia madaraka au mamlaka yao vibaya, kuhakikisha dhana ya uwajibikaji na utawala bora inaendelea kuzingatiwa na kuleta tabasamu ambalo Rais wa Dkt.Samia amekusudia.
Sita ni ufanisi na utendaji utakaosaidia uwajibikaji na nidhamu kazini, utekelezaji kwa wakati na tathmini ambayo itapima malengo na kufuatilia kile ambacho tunakifanya na kupima malengo kama yamefikiwa kwa kuyafanyia tathmini na kufuatilia eneo gani linastahili marekebisho.
Saba ni kuzingatia maslahi na haki za watumishi ikiwemo pia kuwapa fursa ya mafunzo, kuwaongezea ujuzi na weledi, huku akisisitiza haitakiwi kufanya kazi kwa kujuana, kuviziana wala kwa kutegena, ambapo amewataka kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na mahusiano yaliyo mema na tija kwa taifa.
Nane ni mafunzo huku akisisitiza wale wanaostahili kwenda mafunzo ikiwa ni programu fupi,warsha,ujuzi au weledi huku akikisitiza lizingatiwe kwa kuwa linaongeza ufanisi na kurahisisha majukumu.
Tisa ni kuzingatia usalama na maadili ya kazi na Kumi ni kuimarisha mawasiliano ya ndani ya taasisi ili kuweza kurahisisha utendaji kazi katika kuwahudumia wananchi, ikiwemo mahusiano kati ya ofisi moja na nyingine, ikiwemo masuala ya kuandikiana barua pepe kati ya ofisi moja na nyingine akisisitiza kuwepo mazungumzo kwanza ya ana kwa ana ili kuweza kurahisisha maamuzi ambayo baadae wayaweke katika maandishi ambapo pia alisisitiza utunzaji wa siri.
Waziri Katambi alimalizia kwa kusisitiza uwepo utaratibu wa kufanya tathmini ya bajeti na rasilimali zilizopo ili kuleta matokeo chanya katika kuwahudumia wananchi ikiwemo ulinzi wa mali na maisha yao.



