Nabii Mkuu Profesa GeorDavie K. Moses azindua vitabu


Na MWANDISHI WETU

NABII Mkuu na Mstahiki Meya wa Amani, Profesa GeorDavie K. Moses, amezindua vitabu viwili—The Kingdom Business na Kuenenda na Viwango vya Utukufu wa Serikali Tukufu ya Ufalme wa Mungu—akisisitiza umuhimu wa jamii kujijenga kiuchumi na kiimani kupitia maarifa ya kusoma vitabu.

Uzinduzi huo ulifanyika juzi katika Kanisa la Ngurumo ya Upako, lililoko Kisongo, wilayani Arumeru, mkoani Arusha na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini kutoka ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Profesa GeorDavie, amesema vitabu hivyo vimebeba hazina kubwa ya maarifa ya kiuchumi na kiimani, yatakayosaidia jamii kubadilika na kupiga hatua kupitia elimu iliyomo ndani yake.

“Ninafuraha kuzindua vitabu hivi muhimu katika ulimwengu wa sasa. Nimeanza kuviandika kwa muda mrefu, lakini kutokana na majukumu mengi ya kiutumishi, ilichukua muda kuvimaliza. Hatimaye sasa viko tayari kwa manufaa ya jamii,” amesema.

Akifafanua kuhusu kitabu cha The Kingdom Business chenye zaidi ya kurasa 900, alisema kinaelezea kwa kina masuala ya uchumi na nafasi ya fedha katika kumtumikia Mungu, kikilenga kuwajengea watumishi wa Mungu na jamii kwa ujumla uelewa wa umuhimu wa nguvu ya kifedha katika kazi za ufalme.

Ameeleza kuwa shughuli nyingi za maendeleo, ikiwemo kazi za kiroho, zinahitaji rasilimali fedha ili kufanikisha utekelezaji wake.

“Hata mipango ya kufanya mikutano ya kimataifa katika nchi kama Ufaransa, Croatia na Ethiopia inahitaji gharama kubwa. Kupitia kitabu hiki, watu watapata maarifa ya namna ya kujiandaa kiuchumi,” alisisitiza.

Kuhusu kitabu cha Kuendana na Viwango vya Utukufu wa Serikali Tukufu ya Ufalme wa Mungu, alisema kinaelekeza namna ya kuelewa misingi, itifaki na utendaji wa kiroho katika ufalme wa Mungu, pamoja na kuwajengea watumishi uwezo wa kukua katika huduma za kinabii.