Na Mwandishi Wetu
NAIBU Kadhi Mkuu wa Tanzania, Sheikh Ally Ngeruko, amewataka viongozi wa dini na waumini kote nchini kusimamia na kuimarisha amani, utulivu na mshikamano, huku akisisitiza umuhimu wa kuwahamasisha vijana kujishughulisha kiuchumi, kuepusha vishawishi vinavyoweza kuhatarisha usalama wa taifa.
Sheikh Ngeruko, ametoa wito huo katika maadhimisho ya Siku ya Kuzaliwa kwa Umoja wa Maimamu na Walimu wa Madrasa, uzinduzi wa basi na gari la wagonjwa la Umoja wa Maimamu na Walimu wa Madrasa (UMATA), Kiwalani, jijini Dar es Salaam, ambapo pia amesema amani ndiyo msingi wa maendeleo yote yanayoshuhudiwa nchini kwa sasa.
"Amani ni kitu muhimu sana katika maisha. Amani hakuna asiyejua raha yake na baraka zake. Mbwembwe zote zinazofanyika katika nchi hii ni kwa ajili ya amani, utulivu na mshikamano," amesema Ngeruko.
Amesema viongozi wote waliohudhuria katika maadhimisho hayo wawe wajumbe wema katika maeneo yao na kuhakikisha wanatumia nyumba za ibada (misikiti) kuelimisha waumini wa rika zote, wazee kwa vijana kuhusu fadhila na ubora wa kulinda amani ya nchi.
Pia ametahadharisha endapo misikiti na taasisi za kidini zitasita kutekeleza wajibu huo wa kuhubiri amani, taifa linaweza kuingia kwenye changamoto kubwa ya kiusalama.
"Tukitoka hapa tukahimize amani, tukahimize watu kujishughulisha kwa sababu mengine yanatokana na watu hawana shughuli. Sasa tukasimamie hayo," alisisitiza Naibu Kadhi Mkuu.
Pia Sheikh Ngeruko amewapongeza UMATA kwa kuwa mfano wa kuigwa na kuanzisha mapinduzi hayo ya kutoa huduma kwa jamii, huku akiwaombea baraka kwa Mwenyezi Mungu ili jambo hilo liweze kuwa endelevu na lenye tija.
"Kitu kikubwa zaidi ni haya yanayofanyika ambayo ndiyo katika jamii yetu yamekuwa hayapo au kwa upungufu mkubwa zaidi. Nini? Huduma kwa jamii. Misikiti yetu inakosa huduma kwa jamii. Misikiti imekuwa kazi yake kuhudumia sala, lakini viongozi wa misikiti hawafikirii kuweka huduma kwa jamii", amesema.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa UMATA, Sheikh Arif Serya, amesema wamezindua magari mawili ambayo ni basi na gari la wagonjwa.
Amesema agari hayo à ina ya Costa ambayo inapakia abiria kwa ajili ya maimamu na walimu wa madrasa kwa juhudi mbalimbali za dini, lakini pia ambulance ambayo inapakia wagonjwa na ikibidi jeneza vilevile kwa ajili ya kupeleka katika nyumba ya kudumu.
Pia katika maadhimisho Arif amesema wameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi Kuu ya UMATA, Maktaba, Kituo cha Mafunzo.





