Na MWANDISHI WETU
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameagiza hatua za haraka kuchukuliwa hususan kusafishwa kwa ufukwe wa Kunduchi, wilayani Kinondoni kutokana na eneo hilo kudaiwa kutumika kwa matukio hatari yakiwemo ya upitishaji wa dawa za kulevya, magendo na ubakaji.
Aidha ameelekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), kufanya uchunguzi wa kina kuhusu taarifa za ufukwe huo kumegwa na kuendelezwa kienyeji na baadhi ya wamiliki wa hoteli zilizo jirani.
Chalamila amesema hayo Julai 23, 2026, alipokagua eneo hilo linalomilikiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) .
Asema kuna timu iliyokuwa imeundwa kufuatilia maeneo muhimu hususan fukwe mkoani humo, ambayo ilibaini fukwe nyingi zina maeneo ambayo hayawezi kuwa na hadhi ya kutumika na wageni kutoka nje ya nchi wanaotarajiwa kuja nchini kushuhudia Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ispokuwa ufukwe huo uliopo Kunduchi.
"Tunajiandaa na AFCO, timu iliyopitia 'beach ' ilibaini maeneo mengi hayawezi kubeba hadhi kwa wageni kutoka mataifa mbalimbali. Eneo hili pekee limeonekana bado liko salama na linaweza kutumika hata kwa mazoezi,"amebainisha Chalamila.
Ameeleza, miezi michache iliyopita ufukwe huo ulikuwa ni ukanda mkubwa wa kupitishia na kuhifadhia dawa za kulevya ambapo baadhi ya hoteli zilidaiwa kutumika kuficha dawa hizo.
Chalamila amesema doria kali zinaendelea kuimarishwa katika eneo hilo pamoja na visiwa vidogo vya Mbudia vilivyopo katika Bahari ya Hindi jirani na ufukwe, kukomesha matukio halamu yaliyokuwa yakifanyika.
"Ufukwe huu bado upo katika uangalizi wa TPDC na TFS. Kuna 'extension' ya hoteli imefanyika katika maeneo haya kienyeji.TAKUKURU fanyeni uchunguzi ni namna gani eneo la serikali linaweza kuwa 'extend' kienyeji", amesema Chalamila.
Pia ameelekeza ufukwe huo ambao ndiyo pekee umebaki kuwa na mazingira ya asili kusafishwa kuanzia leo na kuwekewa usimamizi hususan wa kutambua mipaka yote ya taasisi zinazo miliki chini ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
Amesema eneo hilo pia liwekewe njia ambazo hata wageni watakao kuja kushuhudia AFCON au majeshi kufanyia mazoezi huku akionya kuto kuingiza siasa katika suala hilo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, Katibu Tawala wa wilaya hiyo
Warda Obathany, amesema changamoto kubwa iliyopo katika fukwe wilayani humo ukiwemo ufukwe huo wa Kunduchi ni baadhi ya vijana wa kiume 'Beach Boys' kuwabaka wasichana majini.
"Hawa vijana wanatumia fursa ya kuwafundisha mabinti kuogelea baharini lakini wanapofika kina kirefu cha maji huwabaka na kuwatishia kuwazamisha,"alisema Warda.
Ametaja matukio mengine ni ufukwe huo ulikuwa ukitumika kupitishia bidhaa za magendo, uvuvi halamu na kukithiri kwa vitendo vya uchafuzi wa mazingira.
Wanaopangishwa kelele na uchafuzi wa mazingira.
Warda amesema halmashauri hiyo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, wameendelea kuchukua hatua kali za kudhibiti matukio hayo hatari .
"Katika kudhibiti vitendo vya magendo wenzetu wa Mamlaka ya Bandari, wamepiga kambi katika eneo hilo na kukusanya ushuru,"ameeleza Warda.

