Na MWANDISHI WETU
Fainali za mashindano Makubwa ya kuhifadhi Quraan Duniani , inatarajiwa kufanyika Machi Mosi mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, ambapo mshindi ataondoka na kitita cha sh. milioni 31.2.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Al-Hikma Foundation, Sheikh Nurdeen Kishk, amesema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi .
Amesema pia Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba anatarajiwa kuwa mgeni mwarikwa huku viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa wanatarajiwa kuhudhuria fainali hizo za 26.
Kishk, ametaja zawadi kwa washindi kuwa, mshindi wa kwanza ataondoka na kitita cha sh. milioni 31.2, wa pili sh. milioni 20.8, wa tatu sh.milioni 13, wa nne sh. milioni 10.4 na watano sh. milioni 7.8, huku mshindi mwenye sauti nzuri atajipatia sh. milioni 1.3 na mshiriki mdogo zaidi atapata sh. milioni 1.3 na kila mshiriki atapata kifuta jasho sh. 500,000.
“Maandalizi yamekamilika kwa asilimia 100.Washiriki wataanza kuwasili kesho na siku ya Ijumaa hii watatambulishwa rasmi,”ameeleza Kishk.
Amesema Tanzania itawakilishwa na washiriki watatu, ambapo washiriki watatoka mabara yote duniani na kuwataka waislamu na wananchi wote kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushuhudia namna kitabu kitukufu cha Quraan kilivyo hifadhiwa katika vifua vya washiriki hao.

