Na MWANDISHI WETU
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kipindi cha miaka mitano iliyoishia Desemba mwaka jana na kumshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuipatia wilaya hiyo kiasi cha zaidi ya sh. bilioni 317 za utekelezaji miradi ya maendeleo.
Mpogolo amewasilisha taarifa hiyo katika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, leo ambapo mkutano huo uliipokea na kuipitisha kwa kishindo.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Rais Dk. Samia, alitoa sh. bilioni 317 ambazo zilielekezwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo mingi imekamilika na mingine inaendelea kutekelezwa.
“Katika fedha hizi tulizopatiwa, kiasi cha shilingi bilioni 21 kilielekezwa katika elimu msingi na shilingi bilioni 36 kilielekezwa katika elimu sekondari,”amesema Mpogolo.
Amebainisha kiasi cha sh. bilioni 117 kilielekezwa katika sekta ya afya na sh. bilioni 134 kilielekezwa katika sekta ya barabara .
Mpogolo, ameeleza katika sekta ya elimu wilaya hiyo imejikita katika ujenzi wa majengo ya kisasa ya ghorofa ambapo hadi sasa majengo nane yamekamilika.
Amesema mwaka huu wilaya hiyo kupitia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, inatarajia kujenga shule za ghorofa tano katika kata mbalimbali zikiwemo Kata za Vingunguti na Upanga Mashariki,
“Shule hizi za ghorofa zote zitakuwa na lifti. Ni shule za kisasa na zitakuwa na ofisi za walimu na maabara,”amesema.
Pia, amesema mfumo huo wa majengo ya shule za ghorofa utatumika kwa upande wa shule za msingi.
Kwa upande wa sekta ya afya, Mpogolo ameeleza, hatua kubwa imepigwa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha Mchikichini kilichogharimu sh. bilioni 5.2 na Kituo cha Afya Mzinga ambacho ujenzi wake umegharimu sh. bilioni 3.7 ambacho kiko katika hatua za mwisho kukamilika.
Mpogololo, amesema Halmashaur ya Jiji la Dar es Salaam, itaendelea kutenga fedha kwa kujenga vituo vingine viwili katika Kata za Kisukulu na Mongo la ndege ambavyo vyote vitakuwa katika mfumo wa ghorofa
“Katika eneo la Mnazi Mmoja na Pugu tunatarajia kujenga hospitali zenye hadhi ya wilaya,”ameeleza.
Mpogolo amesema pamoja na masuala mengine, ufanisi huu mkubwa uliopatika ulisaidia Wilaya ya Ilala kuongoza nchi nzima katika matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29 mwaka jana na kumweka Rais Dk. Samia, madarakani.
“Katika matokeo ya uchaguzi nchi nzima Ilala ilikuwa na kura milioni 1.2. Hivyo katika kura zaidi ya milioni 30 ambazo Rais Dk. Samia alipata Ilala tulichangia kura milioni 1.2,”ameeleza Mpogolo.
Akizungumzia uwezeshaji wananchi kiuchimi kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri, Mpogolo, amesema tayai wametekeleza maelekezo ya Rais Dk. Samia kwa kuongeza asilimia tano ya mikopo hiyo hivyo kuwa asilimia 15.
“Tumeweka utaratibu mzuri wa wananchi kupata mikopo hii kwa kuzingatia zaidi vikundi vya wahitaji,”ameeleza.
Kuhusu changamoto, Mpogolo amesema kwa kushirikiana na wataalamu, watendaji na viongozi mbalimbali wilaya hiyo imeendelea kusikiliza na kutatua kero hususan migogoro ya ardhi na mirathi.
“Tutaendelea kushikiriana kutatua migogoro hiyo,”ameeleza mkuu huyo wa wilaya.
Kuhusu kero ya barabara, Mpogolo ameshukuru Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kwa kupitisha kuongeza bajeti ya ujenzi wa barabara za mitaani hasa kwa kiwango cha changarawe.
“Baraza liliongeza bajeti ya barabara kwa asilimia 10-15.Tunashukuru sana,”amesema.
Ameeleza changamoto nyingine iliyo tafutiwa ufumbuzi ni ya wenye viti wa serikali za mitaa kuto kuwa na vitambulisho rasmi.
“Hadi kufikia Machi mwaka huu wenyeviti wote wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, watapatiwa vitambulisho hivyo,”amesema Mpogolo.
KUELEKEA AFCON
Mpogolo amesema wanatambua changamoto ya maandalizi ya kuelekea michuano ya AFCON inayotarajiwa kufanyika hapa nchini mapema mwakani Tanzania ikiwa ni mwenyeji.
“Ilala sisi ndiyo wenyeji zaidi wa michuano hii. Hapa ndiyo kuna uwanja wa ndege, hoteli na kutakuwa na harakati nyingi. Hivyo tumeendelea kuliwekea mikakati suala hilio,”amesema.
Ameeleza ufanisi wa mambo hayo yote unatokana na usimamizi mzuri wa CCM Wilaya ya Ilala, ushirikiano wa kiutendaji baina ya halmashauri chini ya Mkurugenzi Elihuruma Mabelya, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Charangwa Suleiman, wakuu wa idara na wafanyakazi.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Sidde, alipongeza utekelezaji huo wa Ilani uliosheni kishindo kikubwa cha utekelezaji wa miradi
“Kabla ya kuja hapa Chama tulikagua miradi hiyo na tulikaa vikao vyote kujadili hadi kikao cha Kamati ya siasa ya CCM Wilaya. Tuliichambua Ilani hiyo na kuwasilisha mapendekezo tuliyoyaona yafanyike ili kupata ufanisi, kuondoa kero wananchi wetu,”alisema Sidde
Wajumbe wa Mkutano huo wa Halmashauri Kuu waliridhia kuipokea taarifa hiyo ambapo wamesema imesheheni mambo mazuri ya maendeleo hivyo kumpongeza mkuu huyo wa wilaya kwa utendaji.


