Kikosi Kazi Mkoa wa Mtwara Mkawajibike kwa Vitendo Kupinga Usafirishaji Haramu wa Binadamu


Na GREGORY MILANZI, MTWARA

Kikosi Kazi cha Kupambana na Uhalifu wa Usafirishaji Haramu wa Binadamu Mkoa wa Mtwara kimehimizwa kuwajibika kwa vitendo ili kuhakikisha tatizo la usafirishaji haramu wa binadamu linatokomezwa kabisa.

Akizungumza leo, Julai 24, 2026, wakati wa kufunga semina ya siku mbili iliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Luwa, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Mtaki Kurwijila amesema wajumbe wa kikosi kazi hicho wanapaswa kutekeleza kwa vitendo maarifa na ujuzi walioupata kupitia mafunzo hayo.

ACP Kurwijila amesema kikosi kazi hicho kinapaswa kuchukua hatua za mapema za kuzuia uhalifu wa usafirishaji haramu wa binadamu badala ya kusubiri madhara au matukio yatokee ndipo kichukue hatua.

Aidha, amesisitiza kuwa kikosi kazi kina wajibu wa kuielimisha jamii kuhusu namna ya kuzuia uhalifu huo, kuwalinda waathirika pamoja na kushughulikia taarifa au matukio ya usafirishaji haramu wa binadamu katika maeneo yao. Pia amewahimiza wananchi kutoa taarifa kwa vyombo husika pindi wanapobaini viashiria vya uhalifu huo.

ACP Kurwijila amesema changamoto ya usafirishaji haramu wa binadamu bado ipo katika Mkoa wa Mtwara, huku baadhi ya wananchi wakijihusisha na vitendo hivyo kwa kujua au kwa kutokujua. Amesema ni muhimu kwa jamii kukemea na kuacha kabisa kujihusisha na vitendo hivyo vinavyokiuka sheria.

Kwa upande wao, baadhi ya wajumbe wa Kikosi Kazi cha Mkoa wameeleza kuwa watatekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa kuzingatia mafunzo waliyopata. Pia wameomba ushirikiano kutoka kwa wananchi, hususan katika kutoa taarifa na ufafanuzi utakaosaidia kuzuia na kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu.

Semina hiyo ya siku mbili iliandaliwa na CVM kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Sekretarieti ya Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Watu (ATS), kwa ufadhili wa Serikali ya Italia. Mafunzo hayo yamewakutanisha wadau mbalimbali kutoka taasisi za serikali na asasi za kiraia kwa lengo la kuimarisha mapambano dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu.