Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula amewapongeza watumishi wa Taasisi mbalimbali zilizopo chini ya wizara ya Fedha kwa kuonyesha ushirikiano wa pamoja bila kujali vyeo wala tofauti zao.
Luswetula amesema hayo, alipotembelea banda la Wizara hiyo na kujionea shughuli zinazofanywa na watumishi wa sekta mbalimbali zilizopo chini ya Wizara Fedha, wanaoshiriki Maonesho ya Kimataifa ya 50 ya Biashara yanayoendelea katika Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.
Amesema kikubwa alichovutiwa nacho kwa watumishi wa Taasisi za Serikali hasa ushiriki wa Vyuo mbalimbali na taasisi za kibenki kwenye banda hilo, ikiwemo Chuo cha IFM na Benki ya Maendeleo TIB.
Amesema taasisi hizo kwa sasa zimetoka kwenye matumizi ya karatasi na kuingia kwenye mfumo wa kidigitali.
"Ki ukweli kutoka uvungu wa moyo wangu, nimevutiwa sana sana na uchangamfu wa watumishi wa idara zilizopo ndani ya wizara yangu, kwanza kwa mapokezi mazuri, elimu ya uelimishaji kwenye mabanda hasa kwa wananchi wanaofika kupatiwa elimu hiyo, nimewapenda sana hongereni sana", Luswetula.
Aidha amewataka watumishi hao kuendelea kushikamana kwa kila jambo na kuendelea kuyasemea mambo mazuri yanayofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Luswetula amesema Rais Dk. Samia amefanya mambo makubwa na mazuri kupitia miradi mbalimbali ya kimaendeleo ambayo imekuwa kivutio kikubwa kwa Watanzania na wageni kutoka nje ya nchi.
Kwa upande wake Meneja wa Takwimu Mkoa wa Dar es Salaam, David Danga amesema Naibu Waziri wa Fedha Laurent Luswetula amependezewa na kazi nzuri wanazofanya kupitia taasisi yao hasusan kwa utoaji wa taarifa na machapisho mbalimbali zinazowasaidia watunga sera wadau mbalimbali hasa katika kutekeleza mipango ya Dira ya Maendeleo ya 2020-2050.
Pia amesema katika utendaji wa kazi huwa Changamoto hazikosekani, ikiwemo uwelewa mdogo wa watu kutoamini tafiti mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo.
Alisema kupitia maonesho hayo viongozi wa taasisi hiyo wamekuwa wakitumia muda huo kutatua changamoto hizo kwa wananchi wanaofika kutembelea banda lao na kupata taarifa sahihi zilizopo ndani ya NBS pamoja na utendaji wa majukumu yako kwa ujumla.
