Na MWANDISHI WETU
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ametoa agizo kwa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, itenge bajeti ya utekelezaji wa miradi ya nishati safi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Mpogolo, ametoa agizo hilo, katika kikao kazi kilichowakutanisha Wakuu wa shule za Sekondari na wadau wa Mazingira, Ilala, jijini Dar es Salaam.
"Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam mikakati yake imejipanga kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, kila eneo linalohudumia watu 100 linatumia nishati safi naelekeza Halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya nishati safi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali "amesema Mpogolo.
Mpogolo amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo imeelekeza matumizi ya nishati safi ifikapo mwaka 2050 Ilala inaendelea kuunga mkono Kampeni ya Kitaifa ya matumizi ya nishati safi inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan .
Aidha Mpogolo amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan Kampeni yake ya nishati safi ya kupikia katika shule, masoko na maeneo mbalimbali ya huduma za kijamii.
Amesema matumizi ya nishati safi siyo uchaguzi, bali ni wajibu wetu waanze na shule, masoko na taasisi zinazohudumia watu wengi, kulinda mazingira na kuboresha afya za wananchi.
Mpogolo amesema katika Wilaya ya Ilala, shule 10 tayari zimeanza kutumia nishati safi na zingine tayari mikakati ya kuanza kutumia.


