JAB Yapokea Ombi la Kutoa Mafunzo kwa Bloggers Zaidi ya 200


Na MWANDISHI WETU, JAB

Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), imepokea ombi kutoka Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN) la kutoa mafunzo kwa wanachama wake zaidi ya 200 kuhusu Sheria ya Huduma za Habari, maadili ya uandishi wa habari na umuhimu wa kupata ithibati.

Ombi hilo limetolewa Julai 16, 2026 na Mwenyekiti wa Mtandao wa Mabloga Tanzania, Beda Msimbe, alipokutana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, katika mazungumzo yaliyofanyika ofisi za bodi jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya mazungumzo hayo, Wakili Kipangula, amesema bodi imepokea ombi hilo na iko tayari kushirikiana na mtandao huo katika kuwawezesha bloga kupata uelewa wa kina kuhusu Sheria ya Huduma za Habari, maadili ya taaluma na umuhimu wa kupata ithibati.

Wakili Kipangula amesema mafunzo hayo yataanza kutolewa kwa bloggers wenye ithibati ili kuimarisha weledi na uelewa wao wa majukumu ya kitaaluma, kabla ya kuendelea kuwafikia wale ambao bado hawajapata ithibati.

"Wale ambao hawana ithibati watapata fursa ya kuelekezwa kuhusu masharti ya kisheria ya kupata ithibati, ikiwemo umuhimu wa kuwa na sifa zinazotakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari. Wasio na sifa stahiki watashauriwa kujiendeleza kielimu,  wakidhi vigezo vya kupata ithibati," amesema Wakili Kipangula.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, amesema mafunzo hayo yatawasaidia wanachama wa chama hicho kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, maadili, weledi na kuchangia kwa ufanisi katika kuhabarisha umma na kuitangaza Tanzania kupitia taarifa za maendeleo zinazotekelezwa katika sekta mbalimbali.

Amesema ushirikiano kati ya mtandao huo na JAB, utasaidia kujenga uwezo wa bloggers na kuimarisha mchango wao katika sekta ya habari nchini.