Na MWANDISHI WETU
CHUO Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kupitia Shule ya Tiba ya Meno kuendelea kushirikiana na Shirikisho la Madaktari wa Meno Duniani (FDI), katika kutoa elimu ya tiba ya meno na maendeleo ya taaluma hiyo.
Akizungumza katika ziara ya shirikisho hilo chuoni hapo, jijini Dar es Salaam, hivi karibuni, Mkuu wa Shule ya Tiba ya Meno MUHAS, Dk. Ferdinand Machibya, amesema MUHAS itaendelea kuwa na mchango mkubwa katika kuzalisha wataalamu wenye ujuzi kupitia ufundishaji, utafiti na huduma za ushauri wa kitaalamu.
Amesema Shule ya Tiba ya Meno imekuwa ikivutia wanafunzi wa shahada za uzamili na wataalamu kutoka nchi mbalimbali wanaojiunga na chuo hicho kwa mafunzo maalumu na kozi fupi za afya.
Dk. Machibya amesema ziara hiyo inaonesha kuongezeka kwa ushirikiano kati ya MUHAS na washirika wa kimataifa katika kuendeleza elimu ya tiba ya meno na huduma za afya.
Kwa upande wa Rais wa Shirikisho la Madaktari wa Meno Duniani (FDI), Profesa Nikolai Sharkov, alisema Shule ya Tiba ya Meno ya MUHAS ina mchango wake katika sayansi ya afya ya kinywa na meno kwani ni Kituo Bora cha Umahiri katika Sayansi ya Afya ya Kinywa na Meno Afrika Mashariki.
Pia Profesa Sharkov ameipongeza MUHAS na Chama cha Madaktari wa Meno Tanzania kwa mchango wao katika kuimarisha huduma za afya ya meno na kuzalisha wataalamu wenye sifa nchini Tanzania.
Aidha, amewahimiza wanafunzi wa tiba ya meno kuendelea kuwa makini katika masomo yao na kukuza taaluma zao ili waweze kuchangia ipasavyo katika mustakabali wa huduma za afya ya kinywa na meno.


