Idadi ya Wananchi Waliofikiwa Yaongezeka Kutoka 2% Hadi 22%.
Samia Legal Aid yaendelea kutatua migogoro Dodoma
Serikali Imewekeza Fedha na Wataalamu Kuhudumia Wananchi Bure Kisheria.
Wananchi Laki 6 Wanufaika na Msaada wa Sheria wa Mama Samia Dodoma
Zaidi ya wananchi 683,767 katika Mkoa wa Dodoma wamefikiwa na kunufaika na huduma za msaada wa kisheria kupitia Kampeni ya Kitaifa ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign), inayotekelezwa na Serikali chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.
Akitoa tathmini ya utekelezaji wa kampeni hiyo leo Jumamosi, Mei 09, 2026, jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria, Bi. Esther Msambazi amesema mafanikio hayo ni kielelezo cha kiu ya wananchi kupata haki na elimu ya sheria nchini.
Katika tathmini hiyo, Bi. Msambazi amebainisha kuwa kampeni hiyo inaendelea pia katika Mkoa wa Shinyanga lakini kwa Mkoa wa Dodoma pekee, Watu waliofikiwa ni 683,767, jumla ya Migogoro 543 imepokelewa, Jumla ya migogoro 282 imepata suluhu ya kudumu papo hapo na Mashauri 261 bado yapo katika hatua mbalimbali za utatuzi huku yakifuatiliwa kwa ukaribu na wataalamu wa kisheria
Kampeni hiyo imefanikiwa kuwafikia watu wa makundi mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa vyuo, makundi maalum, na wananchi wenye migogoro ya ardhi, mirathi, ndoa, ukatili wa kijinsia, pamoja na kutoa Elimu, matunzo ya watoto na kadhalika.
Mkoani Dodoma, tumeingia hadi kwenye vyuo vikuu vinne na kufanya midahalo na wanafunzi, Hatua hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza uelewa wa sheria kwa vijana na kuongeza mwitikio wa wananchi kutoka asilimia 2 hadi kufikia asilimia 22" aliongeza Mkurugenzi huyo.
Msambazi ametangaza kuwa, kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi, Serikali imejipanga kuzindua rasmi Awamu ya Pili ya kampeni hiyo tarehe 20 Juni, 2026 na kwamba Katika awamu hiyo mpya, Serikali imefanya maboresho makubwa ikiwemo kuongeza muda wa utoaji huduma kutoka siku 9 hadi siku 15 kwa kila mkoa.
Mkurugenzi huyo amesisitiza kuwa kampeni hiyo ni maono ya dhati ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha haki inamfikia kila mwananchi bila kikwazo cha gharama.


