Mbeto ampasha OMO Uchaguzi Mkuu Z'bar Umeshafanyika


Na Mwandishi Wetu,Zanzibar 

Chama Cha Mapjnduzi kimemtaka Mwenyekiti  wa ACT Wazalendo, Othman  Masuoud Othman , kutowapotosha Wananchi kwa kudai  kuna waliojipa Mamlaka   ilahali  kura zilizopigwa  ndizo zilizoiweka Serikali  madarakani .

Kwa muktadha huo, CCM  kimesikitishwa kumsikia kiongozi huyo  akipotosha  ukweli  kuhusu   Uchaguzi Mkuu kama kwamba uchaguzi bado haujafanyika Zanzibar.

Kauli hiyo imetamkwa na Katibu wa Kamati  Maalum  ya NEC Zanzibar,Idara ya Itikadi, Uenezi  na Mafunzo,  Khamis Mbeto Khamis,  aliyesema matamshi ya Mwenyekiti huyo   wa ACT Wazalendo yana    upungufu na  walakin.

Wakati akifungua kikao cha Kamati Kuu ya ACT  Wazalendo Jijini Dar es Salaam, Othman alidai kuna waliojipa Madaraka huku wakishindwa kutenda  haki na  kutotimiza wajibu  stahiki kwa Wananchi. 

Akijibu  madai hayo, Mbeto alisema  hakuna Serikali  Duniani inayojiweka Madarakani ,  bila  kupata ridhaa na idhini ya Wananchi  kupitia ushiriki wao katika  demokrasia ya Uchaguzi. 

Alisema jaribio la  kutaka  kuiaminisha jamii na  dunia ya kwamba  Serikali iliojiweka madarakani , hizo ni  Ngenga , Varange na sarakasi  za  kisiasa , jeuri na ukaidi usio na maana  wala mantiki .

"Tumeshiriki  Uchaguzi Mkuu Dunia nzima ikitushuhudia  .Wagombea Urais ,Ubunge, Uwakilishi na Udiwani wa Vyama vyote waliomba kura wakapigiwa .Chama kilichoshinda kilitangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar  hivyo ni makosa kudai kuna waliojiweka Madarakani"  Alisema Mbeto.

Aidha ,Katibu Mwenezi  huyo alisema CCM imekiita  kitendo cha Othman kupita akidai mshindi amejiweka madarakani,  madai hayo  ni porojo na pambio zisizo na uzito wowote .

"Wenzetu  kwa kutojua na  kutaka kuendekeza malumbano majukwaani wamekuwa  wakibeza maendeleo bila kushirikiana na serikali.  Wananchi wapo  na wanashuhudia  yaliofanyika. Kwa kubeza  kwao wamejikuta wakidondoka  kidemokrasia" Alifahamisha 

Hata hivyo Mbeto alimtaka Othman akubali ukweli  hakuwa na nguvu za kisiasa za  kumshinda mgombea Urais wa CCM,,  ambaye tayari ameleta maendeleo  yaliowaridhisha wananchi   miaka mitano iliopita .

"Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 umeshafanyika na matokeo yametangazwa .Kukaa na kudhani Uchaguzi Mkuu bado  haujafanyika  ni kujidanganya mwenyewe  .Uchaguzi umekwisha , mshindi amepatikana na ameshaunda serikali  "Alisema katibu huyo Mwenezi.