Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mkurugenzi Msaidizi Uratibu wa Msaada wa Kisheria, Lucy Darabe Diganyeck amesema utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia awamu ya pili mkoani Dodoma inafanyika katika Halmashauri zote za Mkoa huo, akitoa wito kwa wananchi wenye migogoro mbalimbali ya kisheria kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na huduma hiyo itakayotekelezwa kwa muda wa siku 15.
Lucy amebainisha hayo jana Mjini Dodoma wakati akieleza kuhusu maendeleo ya kampeni hiyo ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia iliyoanza kutekelezwa mkoani humo tangu Mei Mosi 2026 na ikitarajiwa kufika ukomo wake Mei 15, 2026, akibainisha kuwa lengo la kampeni hiyo ni kutoa Msaada wa Kisheria, Elimu kwa wananchi pamoja na kutoa usaidizi katika masuala ya uandishi wa nyaraka mbalimbali za Kisheria.
"Dhumuni la kampeni hii ni kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi, kutoa ushauri wa kisheria, kuandika nyaraka za kisheria, kusuluhisha migogoro kwa njia mbadala ikiwemo ya ardhi na ndoa pamoja na migogoro mingine ya kisheria na nitoe wito kwa wananchi wa mkoa wa Dodoma kujitokeza kwa wingi hasa wale wenye changamoto za ardhi." alisema Lucy
Aidha, Mkurugenzi huyo, alisema Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia hadi sasa imewafikia wananchi 54,000 kwa siku tatu za awali, wanaume wakiwa 25,000 na wanawake wakiwa zaidi ya 28,000 wengi wao wakiwa wanafunzi, madereva pikipiki, wafanyabiashara ndogondogo pamoja na makundi mengine ya kijamii.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma wameeleza kufurahishwa na ujio wa Kampeni hiyo ya msaada wa kisheria inayotolewa bure na serikali, wengi wakieleza kuhusu changamoto za kiutawala pamoja na migogoro mingine ya kisheria, wakieleza matumaini yao ya kupata huduma bora na usuluhishi kutokana tu na maandalizi na mapokeo waliyoyapata katika Kampeni hiyo Mkoani Dodoma.
.jpeg)

.jpeg)