Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetupa shauri la klabu ya Simba kuhusu uhalali wa mchezaji Mohamed Damaro Camara.
Taarifa iliyotolewa na shirikisho hilo kupitia kwa Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Ndimbo, imeeleza kuwa Simba iliwasilisha malalamiko mbele ya Kamati hiyo ikipinga uhalali wa usajili wa Camara, kwa madai unaifanya Yanga kuwa na wachezaji 13 wa kigeni badala ya 12.
Klabu hiyo ilidai usajili wake umekiuka Kanuni ya 62(1) ya Ligi Kuu pamoja na Kanuni Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Kamati katika uamuzi wake, ilisema usajili wa Camara hauna dosari kwa vile habanwi na Kanuni zilizowasilishwa na klabu ya Simba.
Uamuzi kamili wa shauri hilo utatumwa kwa mlalamikaji ambaye ni klabu ya Simba.
