Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete April 1, 2026 ametia saini kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha Rais wa zamani wa Algeria, Jenerali Mstaafu Liamine Zeroual, aliyefariki dunia Machi 28, 2026, akiwa na umri wa miaka 84 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Jenerali Zeroual, aliyependwa na kuheshimika, alichaguliwa kuwa rais mwaka 1995 katika kipindi kigumu cha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Algeria. Alianzisha mageuzi ya kisiasa, ikiwa ni pamoja na kuratibu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi.
Hata hivyo alijiuzulu mapema mwaka 1998 kabla ya kumaliza muhula wake wa miaka mitano ili kutoa nafasi kwa mpito wa kisiasa, na tangu hapo aliishi maisha ya faragha bila kujihusisha sana na siasa.
Hadi leo anakumbukwa kama kiongozi aliyetoa mchango muhimu katika kuiongoza Algeria katika kipindi cha mpito na changamoto kubwa za kisiasa na kiusalama.
Akiongea na Balozi wa Algeria nchini, Ghalib Zermane, Dkt Kikwete amesema Algeria na Tanzania imekuwa rafiki wa karibu kwa muda mrefu na viongozi wake wote waliopita wamefanya kazi kwa karibu na viongozi wa Tanzania kuanzia Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hususan katika ukombozi wa Bara la Afrika, akiwataja viongozi hao kama Ahmed Ben Bella, Houari Boumédiène, Chadli Bendjedid, Liamine Zéroual na Abdelaziz Bouteflika.


