Katambi-Serikali kuboresha Reli ya TAZARA


Katika kuendeleza ushirikiano kati ya Tanzania, Zambia na China ulioanzishwa na viongozi wa nchi hizo akiwemo Rais wa kwanza na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius  Nyerere, Kenneth Kaunda wa Zambia na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Watu wa China, Mao Ze Dong, serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeingia makubaliano na China, kujenga na kuiboresha reli ya TAZARA iliyojengwa  kutoka mwaka  1970 hadi 1975.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, wakati wa Kumbukumbu ya Kuwakumbuka Wataalamu 65  wa Kichina walioshiriki ujenzi wa reli ya TAZARA.

Akizungumza katika eneo la makaburi Gongolamboto Jeshini, jijini Dar es Salaam, Katambi amesema msingi wa ushirikiano ulioanzishwa na waasisi wa nchi hizo katika Nyanja ya Uchumi, Siasa, Teknolojia na Utamaduni imeendelezwa na Rais Dkt. Samia, ambapo Watanzania wameshuhudia miradi mbalimbali iliyojengwa na inayoendelea kujengwa ikisimamiwa na wataalamu kutoka nchini China.

Kwa upande wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, James Millya amesema wao kama Wizara ya kisekta wanaishukuru Serikali ya China kwa kuwa na mahusiano mazuri na Serikali ya Tanzania.

Amesema Tanzania inawaheshimu kwani wakati nchi ya China ikiwa aijaendelea kipindi hicho walikuja kusaidia nchi ya Tanzania ambapo sio rasilimali fedha tu ilitumika bali hadi wataalamu mbalimbali walipoteza maisha.

Naye Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amesema serikali ya China inaendeleza uhusiano ulioanzishwa na waasisi wa mataifa matatu ya China ,Tanzania na Zambia huku akiweka wazi ushiriki wa nchi ya China katika miradi mbalimbali ya maendeleo.