Bank of Africa Tanzania yatoa msaada kwa vituo vya watoto wenye mahitaji maalimu


Bank of Africa Tanzania imeendelea kutekeleza sera yake ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwa kutoa kiasi cha shilingi milioni 24 kwa vituo vinne vinavyolea watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu katika juhudi zake za kuboresha maisha ya watoto ikiwa pamoja na chakula na elimu hapa nchini.

Mkuu wa kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Benki hiyo , Nandi Mwiyombella alisema kwamba vituo hivyo vinne vilivyonufaika na msaada huo ni Amani Foundation for Orphanage Centre (Zanzibar), UMRA Orphanage Centre (Dar es Salaam) , Kijiji cha Furaha (Dar es Salaam) na Kalamu Education Foundation (Dar es Salaam)

“Hiki kaisi si kikubwa wala kidogo ila ni sehemu ya sera ya kusaidia jamii , kwa kiasi cha shilingi milioni 24 kila kituo kitapata kiasi cha shilingi milioni 6 kwa ajili ya chakula na vifaa vya mashuleni ili kujikimu kwenye masomo yao kwa watoto waishio kwenye mazingira magumu kwenye hivi vituo,” alisema Mwainyombella

Aliongeza kwamba benki hiyo inatoa wito kwa taasisi zingine za kifedha nchini kuona umuhimu wa kusaidia makundi haya maalum kwenye jamii kama sehemu ya kuendelea kutokomeza umasikini na kuwajengea uwezo watoto ambao ni taifa la kesho.

"Dhamira yetu kama Benki tunathamini misingi ya ukuaji wa pamoja na utu wa mwanadamu," alieleza Nandi Mwiyombella –. "Kwa kulenga kutoa msaada wa mahitaji haya muhimu, tunalenga kuunga mkono juhudi za vituo hivi ili kuendeleza kazi yao na watoto hawa".

Alisisitiza kwamba kabla benki hiyo haijatoa msaada wowote wa kifedha na chakula ni lazima kwanza kuwashirikisha jamii husika kama vile halmashauri na uongozi wa kituo husika ili kuweza kujua mahitaji ni yapi na maeneo gani yanayohitaji msaada .

Kwa upande wake , Meneja Mradi wa Kalamu Education Foundation (KEF) , Dkt Saidy Ally Soudy alishukuru benki hiyo kwa msaada wa fedha na chakula kwa ajili ya watoto waishio katika mazingira magumu.

“Kituo chetu pamoja na mambo mengine pia kinawasaidia watoto waishio katika mazingira magumu pamoja kikiwa na dhamira pia ya kufanikisha ndoto zao kielimu ambapo wanahitaji msaada wa vifaa pamoja na chakula,” Aliongeza Dr Soudy

Kwa upande wake Martha Massawe ambaye ni Msimamizi wa Kijiji cha Kituo cha Furaha alisema kwamba lengo la kituo hicho ni kuwasaidia watoto waishio katika mazingira magumu na kuwasaidia kupata elimu ya msingi na sekondari.

“Tunaishukuru Bank of Africa Tanzania kwa msaada wao kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa kituo hiki ili kuwasaidia watoto wa kitanzania na kilianza tangu mwaka 2002 hapa katika eneo la Mbweni jijini Dar es Salaam,” alisema Bi Massawe

Naye Hamza Ahmed , katibu wa Umra Orphanage Centre , alisema kwamba kituo hicho kinawasaidia watoto waishio katika mazingira magumu kwa ajili ya kuwasaidia na kuwajengea mazingira mazuri kwa ajili ya maisha ya baadaye.

“Tunaipongeza Bank of Africa Tanzania kwa msaada wao huu adhimu kwa ajili ya watoto wa kituo hiki ni sehemu ya msaada amba oni muhimu kwa ajili ya maisha yao ya baadaye kimasomo na kujiandaa kwa ajili ya kujitegemea,” alisema

Mtoto Zuwena Abbas Ali akiongea kwa niaba ya watoto wenzake wanaolelewa katika Kituo Cha Amani Foundation alitoa shukrani kwa Bank of Africa Tanzania kwa kuwapatia msaada wa vitu mbalimbali kutoa Bank of Africa Tanzania.

Bank of Africa Tanzania ilitoa msaada huo wa kiasi hicho cha fedha unaolenga kusaidia utendaji wa vituo vya watoto wenye uhitaji jijini Zanzibar na Dar es Salaam. Mpango huo unaashiria dhamira ya kudumu ya Benki katika uwajibikaji kwa jamii na azma yake ya kuboresha maisha ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Ikitambua kuwa vituo vya malezi vinakabiliwa na changamoto za mara kwa mara katika masuala ya chakula na utendaji, benki iliamua kutoa Shilingi Milioni 6 kwa kila kituo kati ya vinne. Fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa muhimu za kipaumbele na mahitaji ya chakula, zikitoa msaada unaohitajika ili kusaidia upatikanaji wa huduma muhimu.