Katika kuadhimisha kilele cha Siku ya Wanawake Duniani 2026, wafanyakazi wanawake wa mgodi wa Barrick Bulyanhulu walitembelea shule ya msingi ya wanafunzi wenye mahitaji maalum ya Bupamba iliyopo halmashauri ya Nyang’hwale mkoani Geita ambapo waliwapelekea zawadi mbalimbali.
Ofisa Mahusiano ya jamii wa mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Mary Lupamba, alisema ziara hiyo ni sehemu ya utamaduni wa mgodi huo katika kuadhimisha Siku ya Mwanamke Duniani, ambapo wafanyakazi wanawake hutumia siku hiyo kuwafikia wadau mbalimbali katika jamii na kutoa msaada wa kijamii kama ishara ya mshikamano na upendo.
“Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Kampuni inatumia siku hii kama jukwaa la kutathmini na kuendeleza juhudi za wanawake kazini, kusaidia jamii zinayozunguka migodi hususani makundi yenye mahitaji maalum kama haya na kushiriki katika program Kuchochea wanawake kuingia katika mnyororo wa sekta ya madini”,alisema Lupamba.
Naye Kiongozi wa msafara wa wafanyakazi hao, Asmina Matinga akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi za msaada kwa uongozi wa shule hiyo kuwa wafanyakazi wanawake wa mgodi huo wameona umuhimu wa kusherehekea siku hiyo kwa vitendo kwa kuwafikia watoto wenye mahitaji maalum.
Amesema watoto wenye mahitaji maalum wanastahili kupendwa, kuthaminiwa na kupewa fursa sawa kama ilivyo kwa watoto wengine katika jamii “Kuja kwetu kuwatembelea ni ishara ya kuonesha kwamba jamii inatambua haki zenu na mnpaswa kujiamini ili muweze kutimiza ndoto zenu za maisha", amesisitiza.
Kwa upande wake Ofisa Elimu wa Kata ya Kharumwa, Aloyce Masse, amesema Halmashauri kupitia Idara ya Elimu Msingi iliona umuhimu wa kuwaweka pamoja wanafunzi wenye changamoto za kimaumbile kama vile kuona, kusikia, kuongea na wenye changamoto za ngozi ili kurahisisha utoaji wa msaada na huduma maalumu kwao.
Masse kwa niaba ya shule ya msingi Bupambana alitoa shukrani kwa Wafanyakazi Wanawake wa mgodi wa dhahabu wa Barrick Bulyanhulu kwa hatua hiyo ya kuwafariji watoto hao, akisema msaada waliotoa unaleta faraja kubwa na kuwapa hamasa wanafunzi hao kuendelea kusoma kwa bidii na kujiona ni sehemu ya jamii.




