Balozi Mulamula asheherekea mafanikio wanawake Afrika, akemea ukatili wa kijinsia


Kuelekea kilelele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yatakayofanyika  Machi 8, 2026, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa  Afrika kuhusu masuala ya Wanawake Amani na Usalama, Balozi Liberata Mulamula amesema anafurahishwa na mafanikio yaliyofikiwa kwa wanawake wa Afrika ikiwemo kushika nafasi za juu za uongozi yaani urais.

Pia, ameguswa na kukemea vitendo vya unyanyasaji wa  kijinsia, machafuko na vita vinavyoendelea katika Bara la Afrika na kwingineko ambapo waathirika wengi ni wanawake na watoto.

Ameyasema hayo, leo, Nchini Addis Ababa Ethiopia, anakoendelea na majukumu yake ya wanawake kupitia AU, wakati akitoa salaamu kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake ambayo huadhimishwa kila mwaka Machi 8.

"Katika kuadhimisha siku hii adhimu kwa wanawake, ni fursa ya kutafakari tulikotoka tulipo na tuendako kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu isemayo ‘ Haki, haki. Uwajibikaji kwa Wanawake na Wasichana wote.

"Kama Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Afrika kuhusu masuala ya Wanawake Amani na Usalama, naungana na wanawake duniani kote hususan katika bara letu la Afrika kukemea vitendo vya unyanyasaji dhidi ya jinsia, machafuko na vita vinavyoendelea katika bara letu na kwingineko ambapo waathirika wengi ni wanawake na watoto", amesema.

Balozi Mulamula amesema, Pamoja na kuwakumbuka wanawake hao, wanaoendelea kuteseka, pia ni wakati wa kusheherekea mafanikio tuliyoyapata katika Bara la Afrika kuwa na wanawake wengi waliofanikiwa kushika nafasi za juu za uongozi katika ngazi mbali mbali na Taasisi kadhaa. 

Ameongeza "kubwa zaidi tunasheherekea na kujivunia kuwa na Marais wanawake Afrika, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais Netumbo Nandi Ndaitwa wa Namibia. Kazi na utu tunasonga mbele!! Tuendelee kuziombea nchi zetu na bara letu la Afrika amani, utulivu na usalama wa kudumu".