Ofisi ya Makamu wa Rais na Jiji la Dar es Salaam zakubaliana kuandaa makubaliano kuanzia Kituo cha Kumbukumbu za Muungano


Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam zimekubaliana kuandaa Hati ya Makubaliano (MoU) kuufanya Ukumbi wa Karimjee kuwa Sehemu ya Kituo cha Kutunza Kumbukumbu na Nyaraka za Muungano (Makavazi).

Akizungumza katika kikao baina ya wataalamu wa Ofisi hizo Machi 31, 2026 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Muungano Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Juma Mohammed Salum, amesema makubaliano hayo ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Dkt. Salum amesema Ofisi ya Makamu wa Rais ilipewa maelekezo mahsusi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuanzisha Vituo Vya Kutunza Kumbukumbu na nyaraka Muungano (Makavazi) upande wa Tanzania Bara na Zanzibar ili kusaidia wananchi kuelewa chimbuko na misingi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

“Makubaliano hayo yataweka msingi muhimu katika kutunza historia ya taifa letu kwani ukumbi wa karimjee ni moja ya eneo muhimu na sote kama tunavyokumbuka ndipo ambapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilizaliwa mwaka 1964” amesema Dkt. Salum.

Aidha Dkt. Salum amesema makubaliano hayo pia yatawezesha utunzaji na uhifadhi wa taarifa muhimu za Muungano ambazo ni muhimu kwa ajili ya mustakabali wa kizazi cha sasa na baadae na kuwa hatua hiyo inawezesha wananchi kufahamu manufaa ya Muungano.

“Zipo baadhi ya nchi duniani ikiwemo Ujerumani soko la historia ni muhimu sana kwa wanafunzi wa taifa hilo, hivyo sisi tumeona ni muhimu kutunza historia ya taifa letu kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo” amesema Dkt. Salum.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Bw. Elihuruma Mabelya ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuandaa andiko hilo na kuwa Ofisi yake itatoa ushirikiano unaohitajika ili kufanikisha wazo hilo ambalo ni muhimu kwa mustakabali wa taifa.

“Tunashukuru kwa wazo hili ambalo sisi kama Jiji tutahakikisha linapitia ngazi zote za maamuzi ikiwemo kujadiliwa na kupitishwa katika vikao vya Baraza la Madiwani ili kupata baraka na hatimaye kuanza utekelezaji” amesema Elihuruma.

Aidha Elihuruma alishauri kuundwa kwa kamati ndogo ya wataalamu kwa ajili ya kuratibu mpango kazi utakaondaliwa ambao utaongeza kasi ya utekelezaji wa malekezo yanayotolewa katika ngazi za maamuzi.

Kikao hicho cha siku moja kiliwashirikisha wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa.