Unywaji chai ya moto iliyopitiliza imetajwa ni hatarishi kupata saratani ya koo


NA MWANDISHI WETU

Wananchi wametakiwa kujenga utaratibu wa kupima afya zao ili kujikinga na magonjwa mbalimbali ikiwemo saratani ya koo.

Hayo amebainisha Daktari Bingwa wa Saratani wa Hospitali ya Ocean Road, Sadiq Siu, amesema tatizo linapogundulika mapema inakuwa ni rahisi kutibika.

Akizungumzia kuhusu saratani ya Koo, Dk. Sadiq amesema watu wanaopendelea kutumia vinwaji vya moto kupita kiasi wako hatarini kupata saratani koo.

Pia amesema saratani ya koo inaweza kusababishwa na uvutaji wa sigara, ugoro, unywaji pombe, unene uliopitiliza, chai au uji wa moto uliopitiliza. 

"Kinachotokea ni kuwa inakwenda kusababisha eneo lile kuzizindua zile seli zianze mabadiliko na tukumbuke kuwa viungo vyetu vya ndani ya mwili vipo haraka kubadilika ,"amesema.

 Dk. Sadiq amesema mabadiliko hayo yanaweza kuzizindua hizo seli na kuanza mabadiliko ya ufanyaji wake wa kazi na kuanza kusababisha ugonjwa wa saratani.

"Tunapozungumzia saratani tunazungumzia tabia hatarashi ni miongoni mwa tabia hatarashi za kufanya mtu apate saratani ya koo, kuna watu ambao wakinywa chai lazima imuunguze hiyo nayo si tabia nzuri ni hatarishi," amesema.

"Zile seli zinavyobadilika zinaanza kukua kwa kasi kuliko kawaida matokeo yake yanatengenezeka uvimbe na ule uvimbe unasukuma kuta za koho alafu unapunguza ukubwa wa eneo chakula kinavyopita na inapotokea namna hiyo mgonjwa anapata shida kumeza na baadaye kupata maumivu," amesema.

 Pia amesema saratani ya koo inawahusisha sana watu wenye umri mkubwa kuanzia miaka 40 na kuendelea ndio kundi lilo hatari zaidi kupata ugonjwa huo ikilinganishwa na watu wenye umri mdogo.

"Njia ambazo zinaweza kumtibu mgonjwa wa saratani ya koho ni njia ya upasuaji,tiba kemia lakini pia tunaweza kutibu ugonjwa wa saratani ya koo kwa kutumia mionzi", amesema.

 Dk.Sadiq amesema ugonjwa huo umeonekana ukienea zaidi kwenye maeneo ya Kaskazini na Kaskazini Mashariki ikiwemo Tanga, Kilimanjaro, Dar es Saalam.