Na OWM - TAMISEMI, Muheza
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, amemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, kuwapumzisha kutekeleza majukumu yao watumishi 14 wa Halmashauri hiyo ambao wanatuhumiwa kusababisha changamoto zilizokwamisha ujenzi wa jengo la utawala.
Shemdoe amewataja watumishi hao wanaosimamishwa kazi kupisha uchunguzi ni Afisa Hesabu Mwandamizi Rajabu Mushi, Mhandisi wa Kilimo Mkuu Abdallah Mohamed Jaha, Afisa Ugavi Msaidizi Shukuru Marandu, Afisa Rasilimaliwatu Jesca Luvigo, Mhandisi Careen Meela, Mkuu wa Idara ya Manunuzi Mwangaza Kusenge, Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi Pilly Sindanguru na Kaimu Mkuu wa Idara ya Huduma za Sheria Angela Mwapachu.
Amewataja wengine kuwa, ni Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Sempindu Mgaya, Mkuu wa Kitengo cha Michezo, Utamaduni na Sanaa Msafiri Nyaluva, Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi Zautuni Abdallah, Mkuu wa Kitengo cha Uhifadhi wa Mazingira Issa Msumari, Mhasibu Nasibu Mashanjala na Mhasibu Moses Mpembo.
Shemdoe amefafanua kuwa, yeye pamoja Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete waliunda timu ya uchunguzi, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Mkuu, ambaye wakati wa ziara yake ya kukagua mradi wa jengo la utawala Muheza alibaini uwepo wa changamoto katika utekelezaji wa mradi huo na kuelekeza wachukue hatua za haraka kubaini wahusika na kuwachukulia hatua stahiki.
Shemdoe amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, kuunda Kamati ya Uchunguzi wa Awali, kuwachunguza watumishi hao wanaotumiwa kukwamisha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo la utawala.
Pia, amemtaka mkurugenzi huyo, kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi waliotajwa na ambao hawakutajwa endapo watabainika kuhusika katika kusababisha changamoto katika utekelezaji wa mradi huo baada ya uchunguzi wa awali kukamilika.
Aidha, kwa wahusika waliotajwa katika taarifa za awali wasio watumishi Umma, Shemdoe amevielekeza vyombo vinavyohusika na uchunguzi ikiwemo Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchukua hatua stahiki dhidi yao.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema, majukumu ya ofisi yake pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI ni kuratibu masuala ya utumishi wa umma nchini, kwani Ofisi ya Rais UTUMISHI ndio mwajiri mkuu anayewapangia watumishi vituo vya kazi na vituo hivyo vinasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI.
Kikwete ameongeza kuwa, linapotokea jambo linalohusu masuala ya kiutumishi yeye Waziri wa UTUMISHI na Waziri wa TAMISEMI wanahusika kusimamia na kuratibu utekelezaji wa majukumu ya watumishi wa umma na ndio maana Mhe. Waziri Mkuu Dkt. Nchemba amewaelekeza kushugulikia changamoto hiyo ya utekelezaji wa Mradi wa jengo hilo.
Maelekezo aliyoyatoa Waziri Mkuu kwa mawaziri hao, yalitokana na kubaini uwepo wa changamoto ya upotevu wa nondo 700 zenye thamani ya Shilingi 9,200,000.00 zilizonunuliwa kutoka Saifi Store, upotevu wa marine board 192 zenye thamani ya Shilingi 7,800,000.00, upotevu wa mifuko ya saruji 300 yenye thamani ya shilingi 4,400,000.00, kufanyika malipo ya kiasi cha Shilingi 110,600,000.00 kwa mhandisi mshauri Edge Engineering and Consulting Limited bila uwepo wa Mkataba na Shilingi 343,900,000.00 kutumika nje ya mradi kwa kulipana posho.





Social Plugin