Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Ilala yaridhishwa utekelezaji wa miradi


Na MWANDISHI WETU

 Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Ilala, imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kumshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza fedha nyingi za miradi hiyo wilayani humo.

Akizungumza katika zaiara ya kukagua miradi  ya maendeleo,  Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama wa wilaya hiyo, Said Sidde, miradi hiyo ni ujenzi wa Kituo cha Afya Mchikichini, barabara za mitaa ya Lindi, Dodoma na Tanga katika Kata ya Ilala, Daraha la Majumba Sitta-Segerea Kata ya Kipawa, ujenzi wa Shule ya Sekondari Kitunda Relini Kata ya Kitunda na barabara ya Shedapha Bonyokwa.

Sidde amesema Ilala imetekeleza miradi hiyo kwa ubora unaolingana na thamani ya fedha,   akiwataka wakandarasi kuikamilisha kwa wakati.

“Tumepita katika miradi sita muhimu, kamati imejionea na kwa kweli tumeridhidhishwa na utekelezaji wa miradi hii ambayo inaendana na thamani ya fedha. Tunamshukuru Rais Dk. Samia, kwa kutuletea miradi hii, Rais amekuwa akipeleka fedha za miradi hii kila maeneo”, amesema.

Pia Sidde ameelekeza kwa watendaji wa Hamashauri ya Jiji la Dar es Salaam na viongozi wa Kata ya Ilala, kujiandaa na mabadiliko makubwa ya kukua kwa eneo la Kariakoo,   ambapo eneo hilo litatanua shughuli zake hadi katika Kata ya Ilala .

“Tumeona barabara za lami zinajengwa lakini kuna shughuli za gereji zinafanyika katika barabara hizi. Viongozi wa kata ya Ilala hakikisheni barabara hizi zinatunzwa na haziathiriwi na magereji zisije kuharibika mapema. Kariakoo inakua kwa kasi na Kata ya Ilala itakuwa ndiyo Kariakoo ya baadaye hivyo tujiandae mapema kuhakikisha barabara hizi haziathiriki,” amesema.

Aidha Sidde amepongeza ujenzi wa Barabara ya Bonyokwa inayoanzia Shedapha, Masia- Canada kwa kiwango cha zege, ilikuwa ni adha kubwa kwa wananchi, hususan kipindi cha mvua.

“Mimi ninaishi Bonyokwa naifahamu barabara hii, ilikuwa kero kwa kipindi kirefu,  tunashukuru sana halmashauri kwa ujenzi huu kwa sababu wananchi walikuwa wanapata adha kipindi cha mvua,” amesema.

Kwa upande wa Katibu wa CCM Wilaya ya Ilala, Jesica Msangi, amewataka wakandarasi kukamilisha miradi hiyo kwa wakati na ubora unaotakiwa, dhamira ya Rais Dk. Samia ni miradi hiyo kuwanufaisha wananchi.

“Hii ni kazi nzuri inayofanywa na Rais Dk. Samia. Tunamshukuru sana. Kwa kweli tumejionea miradi bora mpaka nakosa maneno ya kusema ,” amesema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amemshukuru Rais Dk. Samia kwa kuelekeza fedha nyingi za miradi katika halmashauri hiyo, Kituo cha Afya Mchikichini  kinatarajiwa kukamilika Aprili mwaka huu kinagharimu sh. bilioni 5.5.

“Kuhusu ujenzi wa barabara katika Kata ya Ilala zitajengwa katika mitaa 26 kwa thamani y a sh. bilioni 23 kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP). Tunamshukuru sana Rais Dk. Samia,” amesema Mpogolo.

Amesema, mradi wa Daraja la Majumba Sita-Bonyokwa utakapo kamilika utaondoa kero ya muda mrefu waliyokuwa wakipata wananchi kuvuka mto msimbazi na kwamba daraja hilo litagharimu sh. bilioni 29.7.

“Ujenzi wa Barabara ya Bonyokwa, masia-Canada, kilometa 0.5 utagharimu sh. milioni 569.1 na unatekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani ya halmashauri. Hii barabara ikiwa ni barabara korofi hivyo kukamilika kwake kwa kiwango cha zege kutaondoa kero kwa wananchi,” amesema.

Kwa upande wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kitunda Relini, Mpogolo alisema ujenzi wake utagharimu sh. bilioni 4.2 ambapo ujenzi wake umefikia asilmia 97 na shule hiyo itakuwa ni ya kisasa.