Hazina Zanzibar yaingia makubaliano na Chuo Kikuu cha Ardhi kuwajengea uwezo na uelewa wa kitaaluma watendaji wa SMZ


Na MWANDISHI WETU

OFISI ya Msajili wa Hazina Zanzibar imesaini hati ya makubaliano ya mashirikiano na Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) Dar es Salaam, yenye lengo la kuwajengea uwezo na uelewa wa kitaaluma watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika masuala ya usimamizi, utambuzi na uhifadhi wa mali za umma, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika kulinda rasilimali za serikali.


Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo katika chuo hicho kilichopo Makongo, Msajili wa Hazina Zanzibar, Waheed Ibrahim Muhammad Sanya, amesema ushirikiano huo ni wa kimkakati na unalenga kuimarisha uwezo wa watendaji wa serikali katika kusimamia mali za umma kwa kuzingatia misingi ya kitaaluma na mifumo ya kisasa.


Amesema eneo la kwanza la mashirikiano ni katika utafiti wa kitaaluma, akibainisha kuwa Zanzibar bado ina upungufu wa taasisi zinazotoa mafunzo maalumu yanayohusu masuala ya ulinzi na usimamizi wa mali za umma. 


"Makubaliano haya yamelenga kuziba pengo hili kwa kuwapatia watendaji wetu taaluma zitakazowawezesha kulinda mali za serikali kwa ufanisi," amesema.


Aidha, amesema Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia mali mbalimbali za serikali ikiwemo barabara, majengo na miundombinu nyengine, ambayo inapaswa kusimamiwa na kutunzwa kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.


“Lengo letu ni kuwajengea watendaji uwezo wa kuitambua rasmi mali ya umma, kwa kuwa zipo taasisi za kimkakati kama za manunuzi na uhasibu, tumeona umuhimu wa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ardhi katika kutumia mifumo na mbinu zitakazowezesha mali za umma kujulikana, kutambuliwa na kusimamiwa ipasavyo,” amesema.


Ameahidi kuwa utekelezaji wa makubaliano hayo utaanza mara moja, huku akisisitiza kuwa yatatoa fursa za mashirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar katika masuala mbalimbali yanayohusu usimamizi wa mali za umma. 


Hivyo, amewataka watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa tayari kupokea taaluma zitakazotolewa na kuzitekeleza kwa vitendo.


Naye Mhasibu Mkuu wa Serikali, Hamad Saleh Hamad, amesema rasilimali za serikali ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya nchi, hivyo ni lazima zitambuliwe na kusimamiwa ipasavyo.


Amesema awali kulikuwepo changamoto kubwa ya watendaji kushindwa kusimamia mali za umma kutokana na ukosefu wa taaluma maalumu, hali iliyosababisha mapungufu katika uandaaji wa taarifa za rasilimali za taifa.


Hamad kupitia makubaliano hayo, watendaji watapatiwa elimu itakayowawezesha kuandaa ripoti sahihi, kutambua mali za serikali na kuzihifadhi kwa ufanisi, hatua itakayosaidia kulinda rasilimali za umma.


Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Evarist Liwa, amesema mashirikiano hayo yamelenga kujenga mahusiano ya kudumu katika usimamizi wa mali za umma kwa kipindi cha miaka mitano.


Amesema chuo hicho kina utaalamu na kada maalumu zinazotoa mafunzo ya usimamizi wa mali zisizohamishika ikiwemo majengo, mitambo na miundombinu mingine.


Ameongeza kuwa chuo hicho kinafanya tafiti mbalimbali zinazolenga kuboresha mifumo ya utunzaji wa mali za umma kwa ajili ya serikali, sambamba na kutoa elimu ya kitaaluma inayohusu masuala hayo.


Amepongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar kwa uamuzi wa kuingia makubaliano hayo, akisema kuwa wakati Tanzania Bara tayari ina mfumo rasmi wa usimamizi wa mali za umma, Zanzibar ina fursa ya kuanza kwa kuweka kumbukumbu na taarifa sahihi za mali zake, jambo litakalosaidia katika ulinzi na usimamizi endelevu wa rasilimali hizo.


Pia Liwa amesema ni imani yake kuwa mashirikiano hayo yataanza kutekelezwa mara moja na kuleta matokeo chanya yatakayopimika kwa kuzingatia malengo yaliyojiwekea pande zote mbili.




Hazina Zanzibar yaingia makubaliano na Chuo Kikuu cha Ardhi kuwajengea uwezo na uelewa wa kitaaluma watendaji wa SMZ Hazina Zanzibar yaingia makubaliano na Chuo Kikuu cha Ardhi kuwajengea uwezo na uelewa wa kitaaluma watendaji wa SMZ Reviewed by Gude Media on 6:08:00 AM Rating: 5

No comments

Note: Only a member of this blog may post a comment.