UNDP Tanzania yawazawadia wanafunzi wajasiriamali 20 zaidi ya Sh.milioni 70 kupitia Programu ya Youth Ignite Student Founders Fellowship



Na MWANDISHI WETU


Wanafunzi wajasiriamali 20 kutoka vyuo vikuu nchini wamepatiwa zawadi za fedha zaidi ya Sh. milioni 70, kufuatia shindano la uwasilishaji wa mawazo ya biashara lililofanyika chini ya mpango wa Youth Ignite Student Founders Fellowship.


Mpango huo ni awamu ya pili, unaotekelezwa kupitia Programu ya FUNGUO iliyo chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) nchini Tanzania, kwa ufadhili wa pamoja wa Serikali ya Uingereza - kupitia Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo ya Uingereza (FCDO), Umoja wa Ulaya (EU) na serikali ya Finland.


Hafla hiyo ya uwasilishaji wa mawazo ya biashara iliwakutanisha pamoja wanafunzi 30 kutoka taasisi za elimu ya juu kutoka vyuo tofauti Tanzania, waliowasilisha mawazo bunifu ya biashara yenye mchango chanya kwa jamii mbele ya jopo la majaji.


Tukio hili limekuwa hatua muhimu katika kuimarisha ujasiriamali na ubunifu miongoni mwa vijana nchini. Mbali na ushindi wa zawadi za fedha taslimu, wanafunzi wajasiriamali pia walipokea msaada wa kitaalamu, ikiwemo mafunzo ya maendeleo ya biashara, ushauri elekezi (mentorship), maandalizi ya kuwafanya wawe tayari kuvutia wawekezaji wapya.


Akizungumza katika hafla hiyo ya kukabidhi, fedha hizo kwa washindi, Mkurugenzi Msaidizi wa Sayansi na Teknolojia kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Harun Makandi, amesema mpango huo unaendana na ajenda ya Serikali ya kukuza ubunifu, utafiti wenye tija kibiashara na ujasiriamali miongoni mwa vijana.


“Mpango huu unaunga mkono moja kwa moja jitihada za serikali za kulea kizazi kipya cha wabunifu na wazalishaji wa ajira mpya kinachotoka katika taasisi zetu za elimu ya juu. Unaakisi mwelekeo wa Tanzania wa kuunganisha sayansi, teknolojia na ujasiriamali katika maendeleo ya taifa", amesema.


Kwa upande wa Naibu Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, John Rutere, jukumu la UNDP nchini Tanzania limejikita katika kuunga mkono Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 (DIRA 2050).


Amesema UNDP imeweka lengo la kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati cha juu kwa kufikia kiwango cha uchumi wenye thamani ya Dola za Kimarekani Trilioni moja ifikapo mwaka 2050.

Rutere amesema programu kama Youth Ignite Student Founders Fellowship ni mifano halisi ya miradi inayoongeza chachu inayowawezesha vijana kwa ujuzi, mitandao ya wawekezaji na mitaji wanayohitaji kujenga biashara zenye uwezo  wa kukua na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa.


Washirika wa maendeleo walichangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha kundi hili la washiriki, Euan Davidson, Kiongozi wa Miradi Endelevu katika Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo ya Uingereza (FCDO), amezungumza kwa niaba ya juhudi za maendeleo za Uingereza, akisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika biashara zinazoongozwa na vijana kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi jumuishi.


Westerwelle Foundation Tanzania na StartHub Africa zilichangia programu kwa kuwapatia washiriki ujuzi wa vitendo wa ujasiriamali, ikiwemo mafunzo ya kuandaa na kuwasilisha wazo la biashara (pitch development) na mawasilisho ya biashara, kuhakikisha wanakuwa tayari kuvutia uwekezaji kabla ya mashindano.


Naye Sanna-Liisa Taivalmaa, Mkuu wa Ushirikiano kutoka Ubalozi wa Finland, amethibitisha kuwa  dhamira ya Finland kuendelea kuunga mkono mifumo ya ubunifu na ujasiriamali wa vijana kama sehemu ya vipaumbele vya ushirikiano wa maendeleo.


Herriet Nairumbe, Mwanzilishi wa Niches Food Products yenye makao Arusha, anajihusisha na uongezaji thamani wa mazao ya pilipili na matunda, amesema fedha hizo zitatumika kununua mashine itakayorahisisha uzalishaji na kuongeza tija.


"Pia tunapanga kuwekeza katika masoko ya mikoa mingine watu wengi zaidi wafahamu bidhaa zetu,” amesema.


Akizungumzia changamoto anazokutana nazo katika biashara yake, Herriet, amesema Changamoto kubwa ni biashara yake kuwa mpya kulinganishwa na bidhaa za kampuni zilizoimarika na zinazojulikana.


"Kupitia programu ya Youth Ignite Student Founders Fellowship, tumeimarisha msingi wa biashara yetu", amesema.


Herriet amesema wamejifunza utunzaji wa kumbukumbu za mahesabu, upangaji wa bei za bidhaa, ujenzi wa timu na huduma kwa wateja — mambo ambayo yanatusaidia kupata na kuwafanya wateja wadumu zaidi.


“Ninaishukuru programu hii kwa sababu imeimarisha uimara wa biashara yetu na kutuwezesha kutengeneza ajira zaidi kwa vijana”, amesema.


Irene Ngatibigwa, Mwanzilishi Mwenza wa Eco Mushroom, kampuni inayojihusisha na uzalishaji wa uyoga na vitafunwa vinavyotokana na uyoga, amesema baadhi ya miundombinu vilimzuia kupanua biashara yake mwanzoni.


“Nilipoanza, changamoto yangu kubwa ilikuwa ukosefu wa miundombinu ya kupanua uzalishaji na kufikia soko kubwa zaidi.


Nilikuwa napata oda lakini sikuweza kuingia mikataba kwa sababu sikuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji ya usambazaji.”


“Hizi Shilingi milioni 6 zitanisaidia kununua vifaa, kuboresha miundombinu ya uzalishaji, na kuajiri vijana zaidi katika uzalishaji na masoko.”


“Kabla ya kujiunga na Youth Ignite Student Founders Fellowship, nilikuwa nafanya biashara kwa mapenzi binafsi tu bila ujuzi rasmi kama vile masoko au namna ya kuwashawishi wawekezaji wapya.


Irene amesema kupitia mafunzo, amejifunza masoko, uwasilishaji kwa wawekezaji, kujenga mitandao na wawekezaji. Ujuzi huo utakuwa muhimu wanapokuza na kupanua biashara zao.


Programu ya FUNGUO ya UNDP inachochea ubunifu nchini Tanzania kwa kuendesha ukuaji wa uchumi kupitia kulea wajasiriamali, kuwezesha upatikanaji wa ufadhili, na kukuza ushirikiano wenye matokeo chanya.


Ikipewa ufadhili wa pamoja na Umoja wa Ulaya, Serikali ya Uingereza, serikali ya Finland, UNDP, FUNGUO inasaidia kuondoa vikwazo ndani ya mfumo wa ubunifu wa Tanzania.


Kuanzia ufadhili mpaka ushauri elekezi, tunawezesha biashara changa na ndogo kwa zana na rasilimali wanazohitaji ili kukua, kustawi, na kuleta athari chanya. 

 










UNDP Tanzania yawazawadia wanafunzi wajasiriamali 20 zaidi ya Sh.milioni 70 kupitia Programu ya Youth Ignite Student Founders Fellowship UNDP Tanzania yawazawadia wanafunzi   wajasiriamali 20 zaidi ya Sh.milioni 70   kupitia Programu ya Youth Ignite Student  Founders Fellowship Reviewed by Gude Media on 5:32:00 AM Rating: 5

No comments

Note: Only a member of this blog may post a comment.