Mbeto : Jussa fanya Siasa safi, acha kumkashifu Mwalimu Nyerere

Mwandishi  wetu, Zanzibar

Chama Cha Mapinduzi  kimetamka  Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Ismail  Jussa  Ladhu akome kumwita Marehemu  Baba Taifa  Mwalimu  Julius  Nyerere alikuwa Kiongozi   mshenzi wakati  amelitumikia Taifa miaka  23 kwa Uzalendo na Uaminifu.

Pia chama  hicho  kimemkanya Jussa asiulinganishe upeo wake  na Mwalimu  Nyerere kwani  hata  Hayati Maalim  Self  Sharif  Hamad hakuwahi kutoa kashfa dhidi ya Marehemu  Mwalimu  Nyerere.

Katibu wa Kamati  Maalum  ya NEC  Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo ,  Khamis Mbeto  Khamis ameeleza hayo akimuonya Jussa asimkashifu na kulidhihaki jina la  Baba wa Taifa  ambaye bado  anaheshimika duniani .

Mbeto  amesema  kama Jussa ni hodari  wa kutukana matusi viongozi  na kuwakebehi , kwanza aanze  kumtukana Marehemu  Maalim Seif ambaye  pia ametangulia mbele ya haki. 

Amesema inashangaza kumsikia  Makamu huyo  Mwenyekiti  wa ACT ,  akimwita Mwalimu Nyerere ni mshenzi  na wenzake   walioazimia kumfukuza CCM  Maalim  Seif na wenzake  sita Mwaka  1987.

"Kinachofanywa na Jussa katika  majukwaa ya Siasa si  katika Siasa safi na  uungwana adilifu  .Siasa za  matusi  na kashfa hazikubaliki katika Taifa  la kiuungwana kama Tanzania", amesema.

Mbeto amedai Jussa akiwa katika kikao cha ndani cha  ACT  Wazalendo,huko  Wilaya  ya Kaskazini  'A'  Mkoa wa Kaskazini  Unguja , pamoja na maneno ya kejeli  amelidhalilisha jina,utu  na hadhi ya Marehemu  Mwalimu  Nyerere.

Hata hivyo, Mwenezi huyo alisema Jussa alikwenda mbali na kuwaita  Viongozi wote  wa CCM ni  majahili ,wezi wa kura ,hawamuhofu mungu pia hawana  imani za  dini .

Hivyo  basi,  Mbeto  alizungumzia Uchaguzi  Mkuu wa Oktoba  Mwaka huu, alisema hauna kisasi na yeyote badala yake wananchi wanajiandaa kutimiza matakwa ya  Katiba ,sheria na demokrasia .

Amesema matamshi ya Jussa katika kikao hicho,  si kwamba tu  yanaweza kupandikiza hasama na  chuki  ,  lakini pia ameitumia  Dini  kuwadhalilisha wenzake  katika ulingo wa   Siasa.

"Jussa ajue kuwa Wazanzibari  hawaiishi kwa  vonyongo,visasi na chuki . Kuwaita wenzake  majahili , hawana imani ya dini ni wazi amekusudia kupandikiza na  kueneza chuki", amesema.

Katibu  Mwenezi  huyo alimtaka Jussa kuacha kumkejeli Mwalimu  Nyerere kwani  licha kuleta  uhuru,kuasisi Taifa, Muungano  ,amejenga misingi  ilioleta Amani, Umoja  wa Kitaifa na Mshikamano uliopo.

Mbeto : Jussa fanya Siasa safi, acha kumkashifu Mwalimu Nyerere Mbeto : Jussa fanya Siasa safi, acha kumkashifu Mwalimu Nyerere Reviewed by Gude Media on 6:51:00 AM Rating: 5

No comments

Note: Only a member of this blog may post a comment.