TWIGA-BARRICK Kinara Kutoa Gawio kwa Serikali 2026, Yatoa Sh. Bilioni 221.9


Ubia kati ya kampuni ya Barrick Mining Corporation na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals Corporation, unazidi kujenga uendelevu wa thamani katika uchumi wa Tanzania ambapo, migodi ya Barrick nchini imetoa gawio la shilingi bilioni 221,907,320,687 kwa Serikali ya Tanzania na kutunukiwa tuzo ya nafasi ya kwanza kwa kuongoza kutoa hisa kubwa mwaka huu. 

Hundi ya gawio hilo (Dummy cheque) imekabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido, katika hafla ya Serikali kupokea Gawio na michango kutoka kwa taasisi na mashirika ya umma (Gawio Day 2026) iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

 Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliipongeza taasisi na kampuni ambazo serikali ina ubia yanayofanya vizuri kwa kutoa gawio na kuongeza tija kwenye ufanyaji wa biashara na uwekezaji kwa maslahi mapana ya nchini.

Katika kipindi cha mwaka wa fedha wa mwaka jana, Barrick-Twiga ilitoa gawio la shilingi bilioni 93.6, mwaka 2022/23 ilishika nafasi ya kwanza kutoa gawio kwa Serikali ya kiasi cha shilingi bilioni 84 ambapo kipindi cha mwaka wa nyuma yake ilitoa gawio ya kiasi cha shilingi bilioni 53.5.

Migodi iliyopo chini ya kampuni ya Barrick na Twiga Minerals nchini ni North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi uliopo katika mchakato wa kufungwa ambapo kwa sasa umebadilishwa kuwa kongani maalumu la Kimataifa la sekta ya madini ijulikanayo kama Buzwagi Economic Special Zone.

Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dk. Melkiory Ngido amesema Barrick na Twiga Minerals mbali na kutoa gawio nono kwa Serikali pia imekuwa ikichangia pato la Serikali kupitia malipo ya tozo mbalimbali katika maeneo yenye shughuli za migodi yake sambamba na kuchangia kukuza uchumi wa Taifa kupitia kulipa kodi, ushuru, magawio, mishahara na malipo kwa wazabuni wa ndani tangu ilipoanzisha ubia na Serikali mwaka 2019 .

Aliongeza uwekezaji wa Barrick kupitia utekelezaji wa mkakati wake endelevu, zaidi ya kuchangia pato la taifa kwa ajili ya ukuzaji uchumi wa nchi pia unaendelea kuboresha maisha ya jamii zinazozunguka migodi yake kupitia ufanikishaji wa miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR), hususan katika sekta za elimu, afya, maji safi na uboreshaji wa miundombinu ya barabara.

Uwekezaji wa Kampuni ya Barrick nchini pia unaendelea kukuza biashara za ndani kwa kunufaisha Wazabuni na wakandarasi wazawa inaofanya nao kazi na kuongeza wigo wa ajira nchini za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

Mafanikio yanayozidi kupatikana kutokana na ubia wa Barrick na Twiga nchini ni kielelezo cha uchimbaji madini endelevu unaoweka uwiano baina ya uwajibikaji wa kiuchumi, kimazingira na kijamii.

 Kwa upande wake , Waziri wa Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo amesema kwamba siku ya Gawio Day ni muhimu kuendelea kujithamini katika juhudi za mageuzi ya kiuchumi na kimkakati,  kuendana na Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2020-2050.

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo ya Gawio Day ambayo ilikuwa na kauli mbiu “Uwekezaji wenye matokeo ya nguvu ya ushindani wa Dira 2020-2050 , Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema kwamba tukio hilo ni mara tatu na muhimu kwa sababu Rais Dk. Samia suluhu Hassan kulipa uzito kutokana na umuhimu wa michango na gawio la hisa kwa uchumi wa na uwekezaji wa taifa.

Aliongeza kwamba mashirika ya umma na makampuni ambayo yapo nchini yana mchango mkubwa kwenye kukuza na kuboresha huduma za kijamii kwa watanzania pamoja na kuchangia kwenye mfuko mkuu wa serikali.