Serikali ya China Itadumisha Uhusiano na Tanzania Sekta ya Mawasiliano


Na MWANDISHI WETU

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kiteknolojia kati ya Tanzania na China,  kuchochea maendeleo ya uchumi wa kidijitali na kupunguza pengo kati ya mijini na vijijini.

Akizungumza katika hafla ya Jionee Maonesho ya Teknolojia ya Juu ya China katika Kituo cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki (EACLC), Dar es Salaam, amesema  mchango wa China umekuza ubunifu na uchumi wa Tanzania,  katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, ushirikiano kati ya Tanzania na China umebadilika kutoka miradi ya miundombinu ya kawaida hadi kufikia maendeleo ya teknolojia za kisasa.

Amesema miradi hiyo imejumuisha upanuzi wa mawasiliano vijijini, matumizi ya akili bandia (AI), nishati jadidifu na maendeleo ya mijini, hali iliyosaidia kuboresha huduma muhimu katika jamii.

“Tumeona mifumo ya nishati ya jua, suluhisho za AI na mifumo imara ya kilimo cha kisasa. Teknolojia hizi zimefungua fursa kwa wakulima na wafanyabiashara wadogo katika kila kona ya nchi,” amesema Kairuki.

Kairuki alisema matumizi ya teknolojia kama uchunguzi wa magonjwa kwa kutumia AI na majukwaa ya elimu ya mbali yamesaidia kupunguza tofauti za huduma kati ya maeneo ya mijini na vijijini.

Amesema katika sekta ya nishati, teknolojia za kijani kama mifumo ya sola na uhifadhi wa nishati zimeiwezesha Tanzania kusogeza mbele lengo la kuwa na umeme wa uhakika kwa matumizi ya nyumbani, vituo vya afya, shule na shughuli za kilimo.

Kairuki amesisitiza haja ya kubadilisha maonesho ya teknolojia kuwa matokeo halisi kwa kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi, pamoja na kuweka ruzuku maalumu zitakazochochea uwekezaji.

Pia Kairuki amesema  umuhimu wa kuwekeza katika uhamishaji wa teknolojia na maendeleo ya ujuzi kwa kuanzisha vituo vya pamoja vya mafunzo na programu za mafunzo kazini ili kuwawezesha wahandisi, mafundi na wajasiriamali wa Kitanzania kushiriki kikamilifu katika ubunifu na uendelezaji wa teknolojia.

“Tunahitaji kuona ubunifu wa kijani ukizalisha matokeo yanayopimika, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa vijiji vilivyounganishwa na huduma za kidijitali na kuboreshwa kwa maisha ya wananchi,” amesisitiza.

Kairuki amesema kupitia ushirikiano huo, Tanzania inaweza kuvuka vikwazo vya maendeleo ya teknolojia na kujenga mustakabali imara wa kidijitali.

Kwa upande wa Balozi wa nchini Tanzania, Chen Mingjian,   amesema ubunifu wa kisayansi na kiteknolojia ni nguzo ya kimkakati katika kuongeza uzalishaji na nguvu ya taifa kwa ujumla na kuwa nguvu muhimu ya kuboresha ustawi wa wananchi.

Chen alisema hivi karibuni China imepata mafanikio makubwa yenye athari ya kimataifa katika nyanja za teknolojia ya juu.

"Katika Akili Bandia (AI), China imekuwa ya kwanza duniani kwa idadi ya hati miliki za akili bandia zalishi tangu mwaka 2017. Katika utengenezaji mahiri na roboti, karibu roboti za viwandani 300,000 zilifungwa nchini China mwaka 2024, zikizidi nchi nyingine na kuchangia zaidi ya nusu ya jumla ya dunia", amesema.

Chen amesema China na Tanzania zinafurahia urafiki wa jadi wenye mizizi imara na ni marafiki na washirika wazuri katika hali zote, enzi hii mpya, ushirikiano wao unaendelea kupanuka kwa kasi katika nyanja za teknolojia ya juu kama sayansi, teknolojia na uchumi wa kidijitali.

Pia amesema katika sekta ya habari na mawasiliano, kampuni za China zimeshiriki kikamilifu katika maendeleo ya miundombinu ya mawasiliano nchini Tanzania, ambapo kampuni ya  Huawei imesaidia kujenga mitandao ya 4G na mifumo ya nyaya za mawasiliano ya nyuzi,  inayofunika miji mikuu nchini kote.

"Katika serikali ya kidijitali na utawala mahiri, ushirikiano wetu umeendelea kuimarika. Teknolojia za China zimeisaidia Tanzania kuendeleza mifumo ya serikali mtandao, kuharakisha mabadiliko ya kidijitali katika maeneo kama ukusanyaji wa kodi, usajili wa vitambulisho na utoaji wa huduma za umma na hivyo kuongeza ufanisi wa kiutawala na utoaji wa huduma", amesema.