Na MWANDISHI WETU
Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba amesema mfumo wa Kidijitali wa kutoa huduma za mafuta na gesi PUMA PRIS ni hatua muhimu ya kuimarisha uchumi wa kisasa unaotegemea teknolojia ndani ya sekta ya mafuta nchini.
Salome amesema hayo, katika uzinduzi wa mfumo huo wa Kampuni ya Puma Ernegy Tanzania, Hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.
Amesema sekta ya nishati ni mhimili wa uchumi wa taifa, hivyo matumizi ya mifumo ya kidijitali yataongeza ufanisi wa huduma pamoja na kukuza matumizi ya teknolojia nchini.
Salome amesema mfumo huo ni teknolojia ya kisasa ya itakayosaidia kusimamia shughuli za vituo vya mafuta ikiwemo mauzo, malipo, usimamizi wa stoki za mafuta na taarifa za biashara kwa wakati halisi.
Amesema mfumo huo unalenga kuongeza ufanisi, uwazi na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wateja na kuboresha usimamizi wa biashara za mafuta nchini.
Pia Salome ameipongeza kampuni hiyo kwa kuendelea kuwekeza nchini kupitia ubunifu wa kidijitali, upanuzi wa vituo vya mafuta na uwekezaji katika nishati safi ya CNG.
Amesema mfumo huo unaendana na malengo ya Tanzania ya kujenga uchumi wa kidijitali kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na mkakati wa DESF 2024–2034.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Fatma Abdallah, amesema kutambulisha mfumo huo ni hatua muhimu wa safari yao ya kuendelea kuboresha huduma kwa wateja kwa kuwekeza katika suruhisho la kisasa linalolenga kuleta thamani halisi nchini.
Amesema kampuni hiyo imekuwa ni mshirika mkubwa katika maendeleo ya sekta ya nishati nchini ikiwa na zaidi ya vituo 100 vya kutoa huduma nchini kote, ikiwemo huduma za mafuta ya ndege katika viwanja vya ndege, nishati safi ya kupikia ya
Puma Gas na uwekezaji katika miundombuni na huduma za kisasa ili kuhakikisha wanachangia ukuaji wa uchumi nchini.
"Mafanikio ya kweli huanza na mteja ndiyo maana leo (jana) tunazindua PRIS, PRIS ni programu ya kwanza nchini Tanzania inayowezesha kupata huduma za Puma pamoja na zawadi mbalimbali kupitia matumizi yao ya mafuta na bidhaa za Puma kama vile, oil katika vituo vyote Puma Ernegy Tanzania", amesema.
Fatma amesema kupitia mfumo huo kila mteja atakayenunua mafuta katika vituo vyao ataweza kukusanya alama na kuzitumia baadaye katika kupata manufaa katika mtandao wao na washirika wao.
Amesema uzinduzi huo pia unaungamkono Dira ya Taifa ya kujenga uchumi wa kidijitali, unaolenga kufanya Tanzania kuwa kitovu cha kidijitali katika ukanda wa Afrika.
Pia amesema mfumo huo tayari umepta mafanikio makubwa katika masoko mengine barani Afrika ambapo kampuni hiyo inaendesha shughuli zake, zikiwemo nchi za Malawi, Zimbabwe na Botswana.
Amesema mafanikio hayo yamewapa imani pia Watanzania watanufaika kupitia ubunifu huo.




