RC Ruvuma awataka Wafanyabiashara Kupokea Elimu ya Kodi na Kueleza Changamoto zao

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Ahmed Abbas (kushoto), akipokea zawadi kutoka kwa Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Nicodemas Mwakileme, alipokutana na timu ya Elimu ya Kodi mlango kwa mlango, alipofika ofisini kwa kumjuulisha kuhusu kampeni hiyo, inayoendelea mkoani humo.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Ahmed Abbas, amewataka wafanyabiashara kutoa ushirikianao kwa maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) watakaopita katika maduka yao kuwapa elimu ya kodi na kueleza changamoto zao, zitatuliwe. 

Abbas ametoa wito huo, alipokutana na maofisa wa TRA waliofika ofisi kwake kwa lengo la kumjuulisha, kuhusu uwepo timu ya kampeni ya Elimu ya kodi ya mlango kwa mlango, wakiongozwa na Meneja wa mkoa huo, Nicodemas Mwakileme. 

Amesema wananchi wa Ruvuma kutojihusisha na biashara ya magendo, kwasababu vitendo hivyo vinaokesesha serikali mapato ambayo yangetumika kujenga vituo vya afya, barabara na mambo mengine kwa maendeleo ya nchi. 

Kwa Upande wake, kiongozi wa timu hiyo, Ofisa Msimamizi Mkuu wa Kodi, Salim Bakari, amesema kampeni hiyo itaendeshwa kwa wiki mbili katika Wilaya ya Songea, Nyasa, Mbinga na Tunduru.

Bakari amesema lengo la kampeni hiyo ni kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu masuala ya kodi na kuwahamasisha  wananchi wa mipakani kutojihusisha na magendo kwa kuwaelezea athari za magendo na njia sahihi za kuingiza na kutoa bidhaa nchini.

Naye, Kaimu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Ruvuma, Alhaji Issa Mzee ameipongeza TRA kwa kuja na kampeni hiyo itawasaidia wafanyabiashara kueleza changamoto zao zitatuliwe.

Mzee amewasihi wafanyabiashara kuwapa ushirikiano maofisa hao kwa kulipa kodi kwa wakati, ili isaidie katika kujenga vituo vya afya, barabara na mambo mengine ya maendeleo.

Mmoja wa wafanyabiashara waliotembelewa na maofisa hao, Olita Alfred, amesema ameifaidika na elimu hiyo na amejifunza umuhimu wa kutumia mashine za EFD, kupata rekodi sahihi za mauzo yao na kusadia kupata makadirio sahihi ya biashara zao.