Na MWANDISHI WETU, Morogoro
Watumishi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia katiba, sheria, kanuni na taratibu na kuepuka lugha zozote za
uchochezi zinazoweza kuleta uvunjifu wa amani na kuhatarisha maisha ya
Watanzania.
Hayo yamesemwa Aprili 11, 2026 na Naibu
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na wenye Ulemavu), Dkt.
James Henry Kilabuko kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt Jimmy Yonaz, wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi, katika kikao kilichoketi Mkoani Morogoro.
“Napenda kuwaasa, kuzingatia katiba,
sheria, kanuni na taratibu mnapotekeleza
majukumu ya Tume na kuepuka lugha zozote za uchochezi zinazoweza kuleta
uvunjifu wa amani na kuhatarisha maisha ya Watanzania,”alisema Dkt Kilabuko.
Dkt. Kilabuko amesema, taasisi ina malengo
yake, upo uwezakano wa kuepusha migogoro ya ndani na nje ya taasisi inayoweza
kuathiri utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa ufanisi.
Mapema akimkaribisha Mgeni Rasmi,
Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi INEC ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi
wa Tume, Ndg. Ramadhani Kailima alisema kwa sasa Tume inaendelea na zoezi la
uandishi wa Taarifa ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka
2025.
“Tume imekamilisha Uchaguzi Mkuu wa Mwaka
2025 ambao ulifanyika tarehe 29 Oktoba, 2025.
Kwa sasa Tume inaendelea na zoezi la uandishi wa Taarifa ya Uchaguzi
Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2025. Taarifa hiyo baada ya
kukamilika, itawasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”alisema
Kailima.
Aidha, amesema Tume ipo katika maandalizi
ya uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Isimani mkoani Iringa kufuatia kifo
cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. William Lukuvi pamoja na uchaguzi wa
udiwani katika Kata mbalimbali nchini ambazo madiwani wake walifariki.
Katika Kikao hicho cha siku moja pia
kilitumika kwa kufanya uchaguzi wa Katibu wa Baraza hilo ambapo wajumbe
walimchagua Ndg. Mwitaru Keboya kuwa Katibu mpya wa Baraza akichukua nafasi ya
Ndg. Livini Avith ambaye amemaliza muda wake.