Na OWM - TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (OWM-TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe ameelekeza hatua za haraka zichukuliwe kuwarejesha wafanyabiashara wa Soko la Mawasiliano (Simu 2000), kuendelea na shughuli za biashara katika soko hilo ambalo lilipata ajali ya moto iliyoteketeza soko hilo Aprili 04, mwaka huu.
Shemdoe ametoa maelekezo hayo Aprili 10, 2026 alipolitembelea soko hilo na kuridhishwa na utekelezaji wa Maelekezo ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba aliyoyatoa Aprili 6, 2026, alipofika kukagua madhara ya tukio hilo la moto na kuelekeza soko hilo kusafishwa mara moja, kuruhusu wafanyabiashara kuanza taratibu za kurejesha shughuli zao.
“Nimeridhishwa na utekelezaji wa maelekezo aliyotupatia Rais na Waziri Mkuu, hivyo naelekeza haraka iwezekanavyo wafanyabiashara warejeshwe kuendelea na shughuli zao lakini wasijenge vibanda na badala yake waweke meza pamoja na miamvuli ili kujikinga dhidi ya jua na mvua,” amesisitiza Shemdoe.
Shemdoe amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kusimamia kikamilifu maelekezo aliyoyatoa, huku akimtaka Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando kufanya ufuatiliaji wa kila siku ili wafanyabiashara wa soko hilo warejee haraka kuendelea na shughuli zao.
Aidha, katika hatua nyingine Shemdoe ameilekeza DART na Mkandarasi anayejenga soko jipya la Mawasiliano kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa viwango ndani ya miezi minne badala ya sita, wafanyabiashara hao wanaorejeshwa kwa kutumia meza wapate vibanda vya kufanyia biashara.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa huo, Chalamila amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Waziri Mkuu ambayo yanayowezesha urejeshwaji wa haraka wa wafanyabiashara hao walioathirika na ajali ya moto katika soko hilo la mawasiliano (simu 2000).
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando amesema, ameelekeza ndani ya siku tatu kuanzia leo kufanyike zoezi la utambuzi wa wafanyabishara wote kwa majina matatu na vitambulisho ili kuepuka changamoto ya watu kuchukua vibanda na kuwapangisha wafanyabiasharana kuongeza kuwa atahakikisha wafanyabiashara watakaopata mikopo ni wale waliothirika na janga la moto na wenye sifa na stahiri ya kupata mikopo.






