Serikali yakutana na Mjumbe Malaamu wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola


Na MWANDISHI WETU

Ujumbe wa Serikali ya Tanzania ukingozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, imekutana na Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola na Rais wa zamani wa Malawi, Dkt. Lazarus Chakwera.

Katika mkutano wao walijadiliana kuhusu namna Tanzania ilivyojidhatiti katika kudumisha umoja, amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.

Kikao hicho kilifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Aprili 9, 2026 baada ya Mheshimiwa Chakwera kukukutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahamoud Thabit Kombo.

Katika kikao hicho, Profesa Kabudi alimueleza kwa kina Mjumbe huyo Maalumu, kuhusu hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuimarisha demokrasia nchini huku ikiweka msisitizo katika kulinda na kuheshimu utu wa Mtanzania, kuzingatia haki na uwajibikaji, amani na utulivu pamoja na kudumisha umoja wa kitaifa. 

“Tumekutana na Chakwera na tumemueleza mambo mengi kuhusu Tanzania na historia ya nchi hii tangu ipate uhuru mwaka 1961, hali ya siasa na demokrasia nchini, na hatua ambazo serikali inaendelea kuchukua ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa tulivu na kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi jumuishi na kujiletea maendeleo”, ameeleza Kabudi. 

Kabudi ameeleza kuwa kikao hicho kimekuwa kizuri na chenye mafanikio, kutokana na mnumbe huyo maalumu wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola kupata ufafanuzi wa kutosha kuhusu masuala mbalimbali yanayoendelea nchini hususani, katika kudumisha amani, umoja wa kitaifa na ustawi wa Watanzania. 

Mbali na kukutana na ujumbe wa serikali, Chakwera anatarajiwa kukutana na wadau mbalimbali ambapo alikutana na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mstaafu Francis Mutungi na vyama vya siasa vya ACT– Wazalendo, Chama cha National League for Democracy (NLD), United Democratic Party (UDP), Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), Chama cha NCCR Mageuzi, Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Alliance for African Farmers Party (AAFP) na Chama cha ADA-TADEA. 

Vyama vingine ni Democratic Party (DP), Tanzania Labour Party (TLP), Union for Multiparty Democracy (UMD), United People’s Democratic Party (UPDP), Chama cha Kijamii (CCK), Demokrasia Makini, Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Katika ziara yake hiyo, Chakwera anatarajia pia kukutana na Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025 na baada ya Uchaguzi Mkuu, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande, Waziri Mkuu Mstaafu na Makamu wa Kwanza, Jaji Joseph Warioba, Jumuiya zisizo za Kiserikali, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Mhe. Jaji George Joseph Kazi na  Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo,  Othman Masoud Othman.

Viongozi wengine ni Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jaji George Masaju, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Balozi, Dkt. Asha-Rose Migiro. 

Aidha, Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, atakutana na Rais  Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Maoinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete.