Ofisa Elimu Sekondari Dk. Mussa apewa tuzo ya elimu


Na HERI SHAABAN

OFISA Elimu Sekondari Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, Dkt. Mussa Ally, amepewa tuzo kwasababu ya usimamizi mzuri katima Idara ya Elimu Sekondari, ukiwemo shule za sekondari Ilala kufanya vizuri.

Tuzo hiyo imetolewa katika Mahafali ya kwanza ya kidato cha sita shule ya Mvuti Sekondari,  Wilayani Ilala  ambapo  wanafunzi 48 walipewa vyeti vya kuhitimu kidato cha sita. 

Akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa shule hiyo, Gasper Mwaipopo, amesema wamemkabidhi tuzo kutokana na mchango wake mkubwa kumsaidia Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika  Sekta ya elimu Idara ya Elimu Sekondari, amefanya mambo makubwa ya ufaulu na kukuza taaluma wilayani humo.

Mwaipopo amesema shule za Wilaya ya Ilala kiwango cha taaluma kimeongezeka na sasa kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Maberya, idara ya Sekondari imejenga shule za Sekondari za kisasa zimekamilika na zingine zinajengwa kiwango cha magorofa. 

"Tuzo hii tumemzawadia mkuu wetu wa Idara ya Sekondari ni alama tosha mchango mkubwa anaofanya wilayani Ilala katika idara ya sekondari kwa kushirikiana na Serikali "amesema Mwaipopo.

Akizungumzia mahafali hayo, Mwaipopo amesema wanafunzi 48 wanatarajia kufanya mitihani yao ya taifa hivi karibuni ambapo wanafunzi hao wamefanya vizuri katika mitihani yao kujipima.

Kwa upande wake Ofisa Elimu Sekondari Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam Dkt. Mussa Ally, ameipongeza shule hiyo kwa kufanya vizuri katika mitihani yao ya kujima Moko hivi karibuni na kuwataka wanafunzi wote waongeze bidii watapata daraja kwanza 'Division one'.

Dk. Ally amewataka wanafunzi hao wakajiandae vizuri kwa mitihani yao na kuchangamkia fursa za masomo mbalimbali. 

Aidha amewataka wanapoenda wakawe mabalozi wazuri katika kuitangaza Sekondari Mvuti ambayo hivi karibuni itakuwa ya vipaji maalumu na bweni kwa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo, Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa sana kuwekeza katika shule hiyo.

Naye Diwani wa Kata ya Msongola, Magdalena Thomas, amewataka wazazi wa na walimu wa shule hiyo kushirikiana kwa pamoja na wanafunzi wa kuongeza ufaulu. 

Magdalena amesema kata hiyo, anajivunia kupata shule hiyo ambayo ina wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi kidato cha sita na hivi karibuni inakuwa ya vipaji maalumu na bweni .

Pia amewataka wazazi katika Jimbo la Kivule, kujivunia shule hiyo kazi iliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa Ilani ya CCM katika sekta ya Elimu.