Doris Mollel na Grobal Fund Kuwaendeleza Kielimu Wasichana Waliokatishwa Masomo


Na MWANDISHI WETU

Taasisi ya Doris Mollel kushirikiana na Shirika la Global Fund, zinatarajia kuanza kutekeleza mradi wa kusaidia kuwarejesha shule wasichana wa rika balehe walioondoka nje ya mfumo rasmi kwasababu ya changamoto mbalimbali ikiwamo ujauzito.

Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa na taasisi hiyo katika mikoa 15 ndani ya halmashauri 47 chini ya ufadhili wa Global Fund na utatekelezwa kwa kipindi cha miezi sita nchini ukilenga kuwawezesha  wasichana katika rika balehe na wanawake wadogo waliokatishwa masomo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo wanaokimbia matukio ya ukatili wa kijinsia kwenye makazi yao.

Hayo yamebainishwa, katika kikao kazi cha wadau na maofisa wa Serikali waliokutana kujadili namna ya kutekeleza mradi huo na kuleta matokeo chanya katika jamii na uendelevu wake baada ya ufadhili wa mradi kutamatika.

 Akifungua kikao hicho, Ofisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Wizara ya Afya, Paul John amesema wizara hiyo inatambua na kuthamini michango ya wadau katika utoaji wa huduma za Ukimwi na afua zingine.

"Afua hii ni muhimu kwa ulinzi wa mtoto, sisi kama Wizara ya Afya tunafahamu eneo la wasichana rika balehe bado liko nyuma katika kukabili maambukizi na linaongoza kwa maambukizi.

Naye, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Doris Mollel amesema taasisi hiyo imefanikiwa kuandaa mikutano zaidi ya minne kila mwaka yenye lengo la kujadili namna ya kutatua changamoto kwa vijana.

"Kupitia jukwaa hili na mashirika zaidi ya 100 huwa tunakutana na kujadili changamoto wanazokutana nazo vijana na namna ya kuzitatua ikiwemo upatikanaji wa vyombo rafiki kwa vijana, upatikanaji wa bidhaa za watoto wa kike kwa gharama nafuu na watoto wa kike waliopata ujauzito wanaotamani kurudi shule lakini wameshindwa," amesema

Amebainisha, mradi huo utazishawishi baadhi ya halmashauri kuwa za mfano katika utoaji wa taulo kwa wasichana shuleni.