DC Mpogolo: Mwenge wa Uhuru Wazindua Miradi Saba ya Maendeleo Ilala


Na MWANDISHI WETU

MKUU wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amesema miradi saba ya maendeleo imezinduliwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 Wazo Mwangonda, wilaya ya Ilala yenye thamani ya shilingi bilioni 51,8, na miradi mingine kuwekwa jiwe la msingi. 

Akizungumza katika Dar es Salaam wakati wa kuzindua miradi hiyo Mkuu wa Wilaya Edward Mpogolo ameitaja miradi saba iliyoxunduliwa na kuwekwa jiwe la Msingi ikiwemo afya,sekta ya Elimu,Uwezeshaji Wananchi,Barabara na Maendeleo ya Jamii. 

Mpogolo alisema wakati wa uzinduzi wa miradi hiyo katika mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 Wananchi mbalimbali walijitokeza katika mapokezi hayo ambapo ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka huu ulikuwa unasema kauli mbiu yake Tanzania ni yetu sote,tushikamane kwa pamoja katika kuleta maendeleo "

"Baadhi ya miradi iliyopitiwa na Mwenge huo Mradi wa kitega uchumi DDC Kariakoo unaojulikana kwa jina la DDC Kariakoo One Stop Business Complex wenye thamani ya shilingi bilioni 36.7 ambapo Mradi huo utatoa ajira zaidi 4000' alisema Mpogolo. 

Mpogolo alitaja mradi mwingine Jiwe la msingi barabara ya Mtaa wa Lindi Ilala yenye urefu kilomita 1.015 kwa kiwango cha lami ambayo ni sehemu ya maboresho ya barabara za Ilala CBD yenye thamani ya shilingi bilioni 23.5.

Aidha alitaja miradi mingine Kisima cha maji safi na Salama Ilala Mchikichini,wenye thamani ya shilingi milioni 164.07 mradi huo unahusisha uchimbaji wa kisima kirefu cha mita 80 ujenzi wa mnara wa tanki la maji la lita 10,000 na usambazaji wa maji kwenye mtandao wa DAWASA.

Pia Mwenge ulikagua na kuweka jiwe la msingi Kituo cha Afya Mchikichini ambacho ujenzi wake utagharimu Sh.bilioni 7.45.Mradi huo ukikamilika unatarajiwa kuhudumia zaidi ya wananchi 325,000 kutoka kata sita za Ilala na maeneo jirani, hivyo kupunguza msongamano wa wagonjwa katika vituo vingine vya afya.

Mradi mwingine uliotembelewa na Mwenge wa uhuru ni Shule ya Sekondari Kitunda Relini ambapo Mwenge uliweka jiwe la msingi katika ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Kitunda Relini iliyojengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 4.21.Shule hiyo ya ghorofa itakuwa na madarasa 16, maabara nne za sayansi, maktaba na ofisi za walimu.

Wakati huo huo Mwenge wa Uhuru ulimalizia na mradi wa kituo cha Polisi Bonyokwa chenye thamani ya shilingi milioni 410.

Akizungumza baada ya kutembelea,kukaguwa na kuweka mawe ya msingi katika miradi hiyo Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 Kitaifa Wazo Mwang’onda amepongeza Halmashauri hiyo na ujenzi wa miradi hiyo sambamba na kutoa baadhi ya maelekezo kwa viongozi wa Wilaya hiyo ikiwemo kuongeza matanki katika mradi wa kisima cha maji safi na Salama kilichopo Kata ya Mchikichini.