Na MWANDISHI WETU, Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi kimesema serikali ya Awamu ya Nane Zanzibar inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, itasimamia Sera za CCM na kuendeleza shabaha ziliowekwa na ASP kabla na baada ya Mapinduzi.
CCM imesisitiza pamoja na kutunga Sera na dira ya Maendeleo, hakitasahau kusimamia mkakati wa vyama vya TANU na ASP.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi , Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis akitaja nia ya SMZ ni kuendelea na mpango wake mkakati wa kujenga Nyumba mpya za Kisasa.
Mbeto kwanza alipongeza uamuzi wa Wananchi Wakaazi waliokuwa wakiishi Nyumba za Mjerumani zilizopo Kiwajuni Wilaya ya Mjini ,kwa kupisha Ujenzi wa Nyumba za Kisasa za Maghorofa uendelee.
Amesema malengo ya ASP kabla na baada ya Mapinduzi yalikuwa ni kuinua hali za Maisha ya jamii kiuchumi, kuwapatia makaazi bora, kuimarisha huduma za afya, maji safi ,matibabu na kufikishia nishati ya umeme.
"CCM ni zao la TANU na ASP . Vyama hivyo viliahidi ikiwa vitashika Dola. Kinachoendelezwa na Rais Dk Mwinyi ni Utekelezaji wa Sera za CCM na kusimamia shabaha za Vyama vya Ukombozi", amesema. Mbeto.
Aidha, Katibu huyo Mwenezi ameongeza kusema ni haki ya kila Mtanzania kupata Makaazi ya uhakika, huduma bora za kijamii kama afya, elimu, nakaazi , ysalama na amani.
"CCM kitatekeleza sera zake za msingi kwa kusimamia na kutekeleza shabaha za vyama vya ukombozi. Sera za CCM zitaibadilisha Zanzibar na kuwavutia Wawekezaji kuja na kuwekeza miradi mikubwa ya kimaendeleo ", ameeleza.
Amesema utakapokamilika Mradi wa Ujenzi kwa Nyumba za kisasa kwa Mjerumani ,Kazi hiyo itafanyika katika nyumba za Kilimani ikiwemo kujengwa nyingine katika maeneo ya Mashamba .
"Maendeleo yatafike Mjini na Mashamba .Kutajengwa makaazi ya kisasa, Shule ,Madaraja na Masoko Mjini na Mashamba", amesisitiza.
Pia Mbeto amesema Serikali Awamu ya kwanza ilijenga nyumba za kisasa Michenzini na Kilimani . Nyingine zikajengwa Bambi, Mkwajuni, Mkokotoni na Makunduchi kwa Unguja"Alisema
Hata hivyo amesema nyumba kama hizo pia zilijengwa Pemba maeneo ya Mkoani, Wete, Micheweni, Kengeja na Chakechake.
