Yaja na programu ya kuwajengea uwezo wanafunzi wa sekta ya madini UDSM
Kampuni ya Barrick nchini imeendelea kufanikisha dhamira yake ya kujenga kizazi kipya cha wataalamu wenye maarifa ya kisasa katika sekta ya madini kupitia programu ya kuwapatia mafunzo wanafunzi wanaosoma shahada ya kwanza ya fani ya madini katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kutumia wataalamu wabobezi na wenye uzoefu kutoka ndani ya kampuni.
Kupitia programu hiyo kwa kushirikiana na Shule ya Madini na Jiolojia (SOMG) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ,wataalamu kutoka Barrick wameendesha ya mafuzo ya kuwajengea uwezo katika tasnia ya madini na jiolojia wanafunzi wa mwaka wa mwisho kwenye shule ya madini.
Akizungumzia kuhusu mafunzo kupitia programu hii Mkuu wa Shule hiyo Profesa Elisante Mshiu alisema yatakuwa ni endelevu kwa kubadilishana uzoefu na wataalamu katika tasnia kutoka Barrick kwa nia ya kuwapatia wanafunzi ujuzi , uelewa wa ndani na jinsi ya kukabiliana na changamoto katika sehemu za uchimbaji na utafiti wa madini kwenye miamba na chini ya ardhi.
Alisema progamu imelenga pia kuwaunganisha wanafunzi na wadau wakubwa katika tasnia ya madini kutoka sekta binafsi ili kuwajengea uwezo na kujiamini ili wanapomaliza masomo yao waweze kuhimili ushindani katika soko la ajira nchini na nje ya nchi na wengine kuweza kujiajiri kupitia taaluma walizosomea.
“Mafunzo haya zaidi yanawapa mwangaza wa aina ya kazi wanazotarajia kukutana nazo pindi wanapomaliza masomo yao , kujua ni kwa jinsi ya kufanya utafiti wa kujua kiasi cha madini kilichopo chini ya ardhi, miamba , namna bora ya kusoma ramani na kuwa na matarajio ya kitafiti na kisayansi zaidi kwenye fani ya Jiolojia,” Aliongeza Profesa Mshiu.
Kwa upande wake , Mkuu wa Idara wa Shule hiyo ya Madini (SOMG) , Dkt Emmanuel Kazimoto alisema mafunzo hayo yanayoendeshwa kwa ufadhili wa kampuni ya Barrick ni fursa ya kipekee kwa wanafunzi wa mwaka wa nne katika shule hiyo katika kupanua uelewa wao kuhusu maswala ya madini , joto la ardhi na elimu ya miamba pamoja na matumizi ya teknolojia kwenye kufanya tafiti za madini chini ya ardhi.
Dkt. Kazimoto alisisitiza kuwa programu itaendelea kufungua milango zaidi wa wanafunzi wa chuo hapo kupenda zaidi masomo ya madini na Jiolojia kwa sababu ya kufundishwa na wadau ambapo wanatoka kweye makampuni makubwa ya uchimbaji madini hapa nchini kama vile Barrick.
“Muhimu ni kwamba wameshawaona wenzao ambapo wamepata kazi Barrick na wengine wamepata kazi nje ya nchini kwa hiyo ni muhimu waendelee kujifunza kwa vitendo zaidi jinsi ya kusoma ramani , ugunduzi wa kiasi ya hifadhi ya madini ambacho kipo chini ya ardhi , jinsi ya kupima joto chini ya ardhi na mambo mengine ya kitaalamu zaidi,” Aliongeza Dkt. Kazimoto.
Amesema kwamba ni muhimu kuendelea kupanua wigo wa ushirikiano kati yao na wadau wa madini kama vile Barrick katika juhudi za kuifanya sekta hii ya madini si tu kwa ajili ya mapato ya nchini lakini pia kupanua mianya ya uelewa wa masomo haya kwa wanafunzi kutoka kizazi hadi kikazi kwa maslahi mapana ya nchini.
Mkufunzi wa mafunzo hayo, Dkt Yann Waku Mpaka , Mjiolojia kutoka kampuni ya Barrick alisema umuhimu wa mafunzo yanayotolewa kupitia programu hii ni jinsi ya kubadilishana na kupeana uelewa , taarifa , ujuzi na uzoefu wa uchimbaji , utafutaji na utafiti kwenye sekta ya madini.
Dkt. Mpaka ameongeza kwamba kuna umuhimu wa kuwajengea uwezo wanafunzi kwenye maeneo ya utafiti , usomaji wa ramani za miamba na jinsi ya kujua joto la ardhi na namna bora ya kufanya shughuli za uchimbaji na utafutaji wa madini kwa njia ya kitaalam zaidi ambayo ni salama pia,na masuala mbalimbali yanayohusiana na tasnia ya madini.
Amesema kuna umuhimu wa kuendelea kuweka mkazo kwenye sayansi na teknolojia nadharia ya uchimbaji na tafiti za madini duniani zimebadilika, uwekezaji mkubwa kwenye vifaa na teknolojia vinawalazimu vijana kwenye sekta hii kujua hasa teknolojia ya kisasa kwenye tafiti na uchimbaji wa madini,” Aliongeza Dkt. Mpaka.
Ibrahim Kamage ambaye ni mtalaamu kutoka Barrick na ni mhitimu wa shule hiyo ya chuo kikuu ya Madini na Jiolojia mwaka 2023 alisema kwamba ni muhimu kwa wanafunzi hao kukuza uelewa wao wa mawasiliano na mahusiano kwa jamii.
“katika fani Jiolojia ni muhimu kwa mtaalamu kujifunza jinsi ya kuwasiliana na watu mbalimbali kuanzia mafundi hadi wanakijiji kwenye maeneo ya uchimbaji ili kupunguza migogoro kwenye jamii na kuondoa dhana potofu kwamba sehemu za migodi ina migogoro na wananchi wanaozunguka migodi hiyo,” Aliongeza Kamage.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake , Paul Maghembe ambaye naye ni mwanafunzi wa mwaka wa nne chuoni alisema kwamba mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa jinsi ya kusoma ramani za miamba , matumizi ya teknolojia na ukusanyaji wa data (takwimu ) kwenye shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini.
Sarah Nestory Musembele ambaye anachukua shahada ya sayansi ya Jiolojia chuoni hapo alisema kwamba ni ndoto zake kwamba anataka kuwa na weledi na kuzingatia maadili ya kazi ya Jiolojia na kuleta mabadiliko kwenye sekta hiyo hapa nchini.

