Al-Hikma yatangaza neema ya kugharamia ndoa ‘mabachela’ 130

Mabinti kuchukua fomu za kuomba wachumba zao kuwalipia mahari


Na MWANDISHI WETU

Al-Hikma  Foundation waandaaji wa Mashindano Makubwa ya  Kuhifadhi Quraan  ya Mabara yote,  imetangaza neema  ya kugharamia   ndoa  130  kwa vijana  wasiyo kuwa na uwezo wa kulipa mahari.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam,  Mkurugenzi wa taasisi hiyo,  Shekh Nurdeen Kishk, amesema  awamu hii  mwanamke anaye taka kuolewa ndiye atakaye chukua fomu ya kuomba mwenza alipiwe mahari na kuozeshwa.

Kishk amesema fomu za kuomba kulipiwa mahari na kuozeshwa kwa mabinti hao zitaanza kutolewa machi 9 hadi Aprili 10 mwaka huu katika ofisi za Al-Hikma, Temeke, Dar es Salaam.

“Wanawake  wanaotaka kuolewa  awamu hii watakuja Al-Hikma kuwachukulia fomu wachumba zao, zijazwe na zirudishwe kusubili hatua nyingine ikiwemo kifanyiwa usahili", amesema.

Kishk amesema awali wanaume ndiyo walikuwa wakichukua  fomu hizo  ambazo zina masharti yanayo mfanya mtu kukidhi vigezo vya kusaidiwa kufunga ndoa, kikiwemo kigezo cha kuwa raia wa Tanzania.

“Huu ni  mwaka  wanne  Al-Hikma Foundation  tumekuwa tukisaidia jamii kuozesha  vijana wa kike na wakiume,  mpaka sasa tumeozesha  ndoa 370,” amesema Kishk.

Amesema  awamu hii Al-Hikma Foundatio  imejipanga kuozesha  ndoa 130 lakini Rais wa   Taasisi hiyo  Sheikh Sharif Al Ahadal ataongeza ndoa 30.

Pia Kishk amesema miongoni mwa vigezo hivyo ni lazima  mwanaume awe na njia za kupata kipato, Kitambilisho cha Taifa (NIDA), barua kutoka kwa Imamu wa msikiti anapoishi.

“Pia mwombaji awe ameposwa na mwanaume awe ameposa, awe mke wa kwanza, mwanaume asiwe unaongeza mke wa pili Kama una mke unataka kuongeza  basi mahari  utalipa mwenyewe,” amesema.

Vigezo vingine ni kukubali ndoa kufungwa jijini Dar es Salaam, wazazi wa mwanamke waridhie ndoa hiyo.