Serikali yatoa tahadhari kuhusu Mafua makali, Uviko 19, Homa ya Dengue na Kipindupindu


Wizara ya Afya imeendelea kufuatilia mwenendo wa magonjwa ya mlipuko, hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa mafua makali ya Influenza na UVIKO-19.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Grace Maegembe, Februari 25, 2026, imeeleza kuwa magonjwa hayo huenezwa kupitia majimaji kutoka kwenye mfumo wa njia ya hewa wa mgonjwa mwenye maambukizi na husambaa wakati wa kukohoa, kupiga chafya au kuzungumza.

Vilevile, mafua makali ya Influenza na UVIKO-19 huweza kuenezwa kwa kugusa mazingira yaliyochafuliwa na majimaji yanayotoka kwa mgonjwa.

Dalili za magonjwa hayo ni homa kali, kikohozi, maumivu ya kichwa na mwili, mafua, kuwashwa koo na uchovu.

Takwimu za ufuatiliaji zinaonesha kuwa, kila mwaka katika kipindi cha mwezi Novemba hadi Aprili kunakuwa na ongezeko la ugonjwa wa mafua makali ya Influenza na UVIKO- 19 hapa nchini na duniani.

Hali hiyo inatutaka kila mmoja wetu kuchukua tahadhari kwa kuzingatia yafuatayo;

i. Kufunika pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya.

ii. Kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono.

ii. Kuepuka misongamano isiyo ya lazima.

iv. Kuvaa barakoa unapokuwa na dalili, unapokuwa karibu na mtu mwenye dalili au ukiwa kwenye maeneo yenye msongamano.

v. Kuzingatia usafi binafsi na wa mazingira.

vi. Kuwahi katika kituo cha kutolea huduma za afya kupata matibabu stahiki, vile vile kuepuka kujitibu au kutumia Antibiotiki bila ushauri wa wataalamu wa afya.

Vile vile, Wizara inapenda kutoa tahadhari ya ugonjwa wa Homa ya Dengue kutokana na maeneo mengi hapa nchini kuwa katika kipindi cha mvua za masika zinazopelekea kuongezeka kwa mazalia ya mbu.

Homa ya Dengue huenezwa na mbu aina ya Aedes ambaye ni mweusi mwenye madoa doa meupe na hupendelea kuuma nyakati za asubuhi, mchana na jioni.

Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na homa kali, maumivu ya kichwa na viungo, maumivu sehemu za macho na uchovu.

Dalili za ugonjwa huo zinafanana na za ugonjwa wa Malaria.

Natoa rai kwa jamii kuzingatia yafuatayo;

i. Kutokomeza mazalia ya mbu yanayowazunguka. Hii ni pamoja na makopo yaliyotupwa hovyo, matairi ya magari, vifuu na kufukia madimbwi kuzuia maji kutuama.

ii. Kujikinga na mbu kwa kuvaa nguo ndefu, kutumia dawa za kufukuza mbu na kuweka nyavu kwenye madirisha.

ii. Kuwahi katika kituo cha kutolea huduma za afya ili kupata huduma stahiki.

Nchi yetu imekuwa katika mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu ulioathiri mikoa yote isipokuwa Kilimanjaro na Njombe.

Kwa kipindi cha takriban mwezi mmoja uliopita, nchi yetu haijapata mgonjwa wa Kipindupindu. Hivyo, napenda kuchukua fursa hii kutambua mchango wa Sekta mbalimbali, Taasisi za Dini, Viongozi wa Jami, Wanahabari, Sekta binafsi, wadau chini ya usimamizi wa Shirika la Afya Duniani na Jamii kwa ujumla kwa juhudi kubwa katika kudhibiti ugonjwa huu.

Vile vile, natambua mchango mkubwa wa wataalamu na watumishi wote kutoka sekta ya afya na sekta nyingine kwa juhudi kubwa katika kukabiliana na mlipuko wa Kipindupindu nchini.

Pamoja na mafanikio haya dhidi ya Kipindupindu, bado tuko katika hatari kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha na uwepo wa maambukizi nchi jirani.

Hivyo, nawasihi kuendelea kuchukua hatua za kujikinga kwa kuzingatia yafuatayo;

i. Kuchemsha maji ya kunywa au kutibu kwa dawa maalumu (aquatab/waterguard) na kuyatunza vizuri wakati wa matumizi.

ii. Kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni kabla ya kula, baada ya kutoka chooni, baada ya kumhudumia mtoto aliyejisaidia na kabla ya kumyonyesha mtoto.

ii. Kuosha matunda kwa maji safi kabla ya kula na kuepuka kula vyakula vya baridi au vilivyoandaliwa katika mazingira yasiyo safi.

iv. Kujenga vyoo bora, kuvitumia na kuviweka katika hali ya usafi nyakati zote, vijidudu vya ugonjwa visingie kwenye maji na chakula.

v. Kuepuka uchafuzi wa vyanzo vya maji kwa kujisaidia, kutupa taka au kutiririsha maji taka.

vi. Kutunza mazingira na kuepuka kutupa taka ovyo

Serikali imejipanga kufuatilia na kutoa huduma dhidi ya magonjwa yote ya mlipuko na itaendelea kutoa taarifa mara kwa mara iwapo kutakuwa na mabadiliko katika mwenendo wa maambukizi au endapo kutahitajika kuchukua hatua zaidi.