Sera ya China Moja na mustakabali bora wa maendeleo, ulinzi na ushirikiano
“Hakuna atakayebadili ukweli kuwa Taiwan ni sehemu ya eneo la China.” Ni Kauli ya msisitizo inayotolewa na Rais wa China, Xi Jinping juu ya uhalali wa eneo la Taiwan na kujibu kauli za upotoshaji za nchi za magharibi kuhusiana na eneo hilo.
Kauli ya Rais Xi Jinping inakwenda sambamba na tamko la kisera na kisheria la Jamhuri ya Watu wa China (PRC) linalotekelezwa na taifa hilo pamoja na kuheshimiwa na mataifa mbalimbali kuwa China ni moja.
Jamhuri wa Watu wa China ni muungano wa China Bara, pamoja na maeneo mengine yenye utawala maalumu unaotokana na historia ambayo taifa hilo limepitia enzi na enzi. Sera ya China Moja inatekelezwa kupitia mifumo miwili ya kiutawala.
Mifumo hiyo ni pamoja na msingi wake ambao ni jiografia, historia na matamko ya kimataifa hususani ya Umoja wa Mataifa (UN). Sera ya "China moja" ni sera inayozungumzia umoja na mshikamano wa nchi ya China katika masuala mbalimbali ya kisiasa, kijamii, na kiuchumi.
Sera hii inahusisha uhusiano wa karibu kati ya China Bara na Taiwan, ambapo China inamiliki eneo hilo na siyo taifa huru kama vyombo mbalimbali vya habari vinavyodai. Sera hii imekuwa msimamo wa taifa hilo kwa miaka mingi juu ya kulinda eneo hilo.
Taiwan imekuwa ikisababisha mzozo mara kwa mara ya kutunishiana misuli ya nguvu za kijeshi dhidi ya China ambayo imekuwa ikisimama imara katika kulinda sera ya China Moja.
Taiwan ni sehemu ya China, na Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC), miongoni mwa majukumu yake ya kipaumbele katika enzi mpya ni kuhakikisha lengo la China kulindwa linafikiwa kwa mafanikio makubwa.
Katika mkutano mkuu wa taifa wa CPC wa 18, mwaka 2012, chama hicho kilitamka kwamba Jamhuri ya Watu wa China itaendelezwa kupitia ujenzi wa ujamaa wenye sifa za Kichina.
Katika mkutano huo, Chini ya uongozi wa kamati kuu ya CPC, hatua mpya na za kibunifu zilipitishwa kuhusiana na Taiwan, katika kuelekea kwenye muungano wa kitaifa.
Taiwan, imeendelea kuwa na dalili za kufuata njia ya kujitenga ikichochochewa mataifa ya nje ikiwemo
Marekani ambayo imekuwa ikikiuka sera ya China Moja, ambayo ilitia saini kuikubali lakini matamshi na vitendo vya nchi hiyo kuleta rabsha na chuki kutaka kuidhibiti China kupitia Taiwan.
“Taiwan ni sehemu muhimu ya ardhi ya China,” alitamka kwa uthabiti, Rais Xi Jingping katika maadhimisho ya miaka 75 ya siku ya taifa, 2024, huku akitoa wito wa kuzidisha ushirikiano wa kiuchumi na kiutamaduni katika Mlango-Bahari wa Taiwan na kupinga harakati zozote za kisiwa hicho kujitenga.
Taiwan ni sehemu ya China, kwa sababu katika zama za kale eneo hilo lilikuwa limeungana na China Bara lakini kukatokea mabadiliko ya tabia nchi ambapo ardhi ilisogea na kuzitenganisha. Eneo la nchi kavu lilokuwa limeunganisha pande mbili hizo, lilizama na kuwa mlango wa bahari, Taiwan ikawa kisiwa.
Utafiti mbalimbali ulifanyika ukihusisha tukio hilo na katika fukukuafukua vitu kama vyombo vilivyotengenezwa kwa mawe, kauri nyeusi na kauri za rangi mbalimbali vilipatikana.
Matokeo ya utafiti yalionyesha nakshi katika vyombo hivyo ni sawa na vile vilivyopo katika China Bara, hivyo kuchukuliwa kuwa ni uhibitisho wa watu wenye utamaduni unaofanana.
Kwa kadri miaka ilivyokuwa ikisonga mbele, tawala za kijadi za China Bara zilituma watu kwenda Taiwan na baadaye wakazi wa pwani ya China Bara, hasa wa Quanzhou na Zhangzhou mkoani Fujiani, walikimbilia au kuhamia Penghu na Taiwan kwa ajili ya kukwepa vurugu za vita.
Mwaka 1335, utawala wa kifalme wa Yuan ulianzisha rasmi idara ya doria na uchunguzi Penghu, kwa ajili ya kusimamia mambo ya raia wa Penghu na Taiwan, na huo ukawa mwanzo wa China kuanzisha mamlaka maalumu ya utawala katika Taiwan.
Hatua kwa hatua mawasiliano kati ya watu wa China Bara na Taiwan yakaendelea siku hadi siku. Mwaka 1628, Fujiani ilipokumbwa na maafa ya ukame, wakazi wa China Bara walienda Taiwan kusaidia, wakijikita katika kilimo.
Tangu hapo Taiwan ikaingia katika kipindi cha uendelezaji mkubwa wa rasilimali na ilipofika mwaka 1684, mkoa wa Taiwan ulianzishwa chini ya mamlaka ya Fujian, na mwaka 1885 hadhi ya Taiwan iliboreshwa kuwa mkoa wa 20 wa China.
Baada ya kuwa koloni la Uholanzi kwa muda mfupi, Taiwan ikawa chini ya ukoo wa Qing wa China, kabla ya kuwa chini ya Japan baada ya taifa hilo kushinda vita vya kwanza dhidi ya China.
Japan ilifanya vita dhidi ya China na kuendelea kuteka visiwa vya Taiwan na Penghu kuanzia mwaka 1931 hadi 1945. Tarehe 9 Desemba 1941, serikali ya China ilitangaza vita dhidi ya Japan na kuapa kuikomboa Taiwan, Penghu na Visiwa vya China Kaskazini vilivyotekwa nyara na Japan.
Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, Japan ilijisalimisha na kuacha udhibiti wa maeneo ambayo ilikuwa imeyachukua kutoka China, na ndipo Taiwan ikatambuliwa kuwa inatawaliwa na Jamhuri ya China (ROC), ambayo ilianza kutawala kwa idhini ya washirika wake Marekani na Uingereza.
Lakini katika miaka michache iliyofuata kulizuka vita vya wenyewe kwa wenyewe China na wapiganaji walioongozwa na Chiang Kai-shek walishindwa vibaya mno na Jeshi la Kikomunisti chini ya uongozi wa Mao Zhedong.
Kutokana na kushindwa katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, Chiang ambaye alikuwa akiongoza chama cha Kuomintang (KMT) na wafuasi wake wanaokadiriwa kufikia milioni 1.5 walikimbilia Taiwan mwaka 1949.
Julai 26, 1945 Marekani na Uingereza walitia saini kutambua China ni moja, katika tamko maarufu la Potsdam ambalo baadaye lilitambuliwa pia na Shirikisho la Nchi za Kisovieti. Mwaka huo huo, Japan nayo ilitia saini makubaliano ya kujisalimisha na kuahidi kutimiza kwa uaminifu tamko la Potsdam.
Oktoba 1, 1949, Jamhuri ya Watu wa China (PRC) ilianzishwa na kuwa mrithi wa Jamhuri ya China (ROC) iliongoza China kuanzia mwaka 1912 hadi 1949 huku azimio namba 2758 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilifikiwa.
Azimio hilo lilijulika “Kurejeshwa kwa Haki Halali za Jamhuri ya Watu wa China katika Umoja wa Mataifa, Oktoba 25, 1971”, linatambua Jamhuri ya Watu wa China (PRC) kama "mwakilishi pekee halali wa China kwenye Umoja wa Mataifa".
Azimio hilo ni hati inayojumuisha kanuni ya sera ya China Moja ambayo mamlaka yake hayaachi shaka na imetambulika miongoni mwa mataifa duniani kote na limekuwa na mchango mkubwa wa maendeleo kwa mataifa mengi ikiwemo Afrika.
Nchi 183 ikiwemo Marekani wameanzisha uhusiano wa kidiplomasia na PRC kwa misingi ya kanuni ya China Moja, kwa nchi kulazimisha kutambua Taiwan kama taifa huru ni uchokozi na kuyumba kimsimamo unaotokana na chuki za kimaendeleo dhidi ya China.
Taarifa ya pamoja ya China na Marekani kuhusu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia iliyochapishwa, Desemba 1978, inasema: serikali ya Marekani inakubali msimamo wa Wachina kwamba kuna China moja na Taiwan ni sehemu ya China.
Pia inasema: Marekani inatambua Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kama serikali pekee ya kisheria ya China. Katika muktadha huo, Wamarekani watashirikiana kiutamaduni, kibiashara, na mahusiano mengine yasiyo rasmi kimataifa na Taiwan.
FAIDA YA SERA YA CHINA MOJA KWA AFRIKA
China imekuwa mtendaji mkuu wa miradi mikubwa ya miundombinu katika nchi nyingi za Afrika. Sera ya China Moja imerahisisha uhusiano wa kibiashara kati ya China na Afrika, na kuanzisha miradi ya barabara, reli, viwanja vya ndege, na bandari, ambayo inasaidia kukuza uchumi wa bara la Afrika.
Sera hiyo imekuwa chachu ya uwepo wa mradi wa BRI (Belt and Road Initiative) ambao umekuwa ni mradi bora wa kimataifa unaohusisha nchi za Asia, Ulaya, Afrika ukiwa na lengo la uimarishaji biashara, ushirikiano wa kiuchumi kwa kujenga miundombinu bora na kukuza uchumi wa kimataifa.
Ushirikiano wa China na nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kumewezesha mataifa hayo kupata mikopo na msaada wa kifedha kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi. China inatoa mikopo kwa nchi za Afrika kwa masharti ya kirahisi kuliko nchi za Magharibi kama Marekani.
Kuvutia Biashara: China imekuwa ni miongoni mwa washirika wakubwa wa biashara wa bara la Afrika. Sera ya China Moja inawezesha ushirikiano wa karibu wa kibiashara, ambapo bidhaa na huduma za China zinapata soko kubwa katika nchi za Afrika. Hii inaongeza fursa za biashara na ajira.
Teknolojia na Ujuzi: China imekuwa mstari wa mbele kutoa msaada wa teknolojia na ujuzi kwa nchi za Afrika. Kampuni za China zimefanya uwekezaji mkubwa katika sekta za teknolojia na ujenzi, na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa Afrika maeneo mbalimbali ya uhandisi, TEHAMA, na uchumi.
Diplomasia na Uhusiano wa Kisiasa: Sera ya China Moja imekuwa na faida katika nyanja ya diplomasia, ambapo taifa hilo limekuwa likishirikiana na nchi za Afrika kuimarisha uhusiano wa kisiasa na kutoa msaada kwa nchi za Afrika kwenye masuala ya kimataifa, ikiwa ni pamoja ndani ya Umoja wa Mataifa.
Kukuza Biashara za Madini: Nchi za Afrika, ambazo ni mataifa yenye rasilimali nyingi, zinapata manufaa kutokana na uhusiano na China katika sekta ya madini. Taifa hilo limekuwa na hitaji kubwa la rasilimali kama mafuta, shaba, na chuma, na kuongezeka kwa biashara ya madini kati ya China na Afrika.
Hivyo, sera ya China moja imekuwa mkombozi wa mageuzi ya kiuchumi na kimaendeleo kwa nchi za Afrika na msimamizi madhubuti wa ulinzi na himaya ya China katika kuwatumikia wananchi wake na kuwa mstari wa mbele katika ushirikiano wa kimataifa na ulinzi wa dunia.
Sera ya China Moja na mustakabali bora wa maendeleo, ulinzi na ushirikiano
Reviewed by Gude Media
on
4:48:00 AM
Rating:
Reviewed by Gude Media
on
4:48:00 AM
Rating:


No comments
Note: Only a member of this blog may post a comment.