Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, ameongoza Kamati ya Maafa ya Mkoa kufika katika kijiji cha Msomera, tarafa ya Sindeni, kata ya Misima, wilayani Handeni, kufuatilia madhara yaliyosababishwa na upepo mkali ulioambatana na mvua kubwa iliyonyesha kwa masaa mawili na kusababisha uharibifu wa makazi, miundombinu na kukatika kwa huduma ya umeme.
Balozi Batilda amesema taarifa za tukio hilo tayari zimewasilishwa kwa Tanzania Red Cross Society na Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuratibu msaada wa haraka kwa wananchi walioathirika. Aidha, ametoa maagizo kwa TANESCO kurejesha umeme na TARURA kushughulikia barabara zilizoharibika.
Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuwa watulivu, kushirikiana na Serikali na kuchukua tahadhari wakati huu wa mvua huku akisisitiza umuhimu wa kupanda miti ili kupunguza athari za upepo mkali na kulinda mazingira.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, amesema kuwa baada ya kufanya tathmini jumla ya nyumba 92 zimeathirika, madaraja matatu, pamoja na taasisi za umma ikiwemo mahakama, kituo cha afya, jiko la shule ya Sekondari Msomera, makanisa pamoja na mabwawa mawili ya Mrunduzi na Msomera.
Wananchi wameishukuru Serikali kwa kuharakisha hatua za msaada, hatua ambayo itawawezesha kurejea kwenye hali ya kawaida haraka iwezekanavyo.





