NA MWANDISHI WETU
DIWANI wa Kata ya Tabata wilayani Ilala, Mkoa Dar es Salaam, Sudi Kassim, amezindua kampeni za Usafi wa Mazingira Mtaa wa Mtambani na kuwataka wananchi kutunza mazingira na kujikinga na magonjwa ya mlipuko.
Sudi ameyasema hayo katika uzinduzi wa kampeni ya Mazingira awamu ya pili iliyoandaliwa na Ofisi ya Serikali za Mtaa Mtambani kwa Kushirikiana na Balozi wa Mazingira Wilaya ya Ilala, Heri Shaban.
Sudi amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeshatoa tahadhari ya magonjwa ya mlipuko hivyo, wananchi wajikinge na magonjwa mbalimbali kwa kufanya usafi katika mazingira yanayowazunguuka.
"Nawaomba wananchi wangu wa Mtambani na Kata ya Tabata kwa ujumla tujikinge na magonjwa ya mlipuko na kunawa mikono kila wakati na kuweka mazingira yetu katika hali ya usafi ", alisema Sudi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo, Abdallah Shomari, amewataka wananchi kuzingatia kanuni za afya na kutunza mazingira kila mmoja ili mtaa uwe kivutio ngazi ya kata mpaka wilaya.
Shomari amesema kwa sasa katika mtaa wake kupitia sheria ndogo za Mazingira na Kamati yake ya Mazingira ya Mtaa wa Mtambani wanafanya ukaguzi mara kwa mara ikiwemo kutoa elimu ya Mazingira kuwachukulia hatua kali wachafuzi wa Mazingira .
Naye Balozi wa Mazingira Wilaya ya Ilala, Shabaan, amesema kampeni ya awamu ya pili ni endelevu inafanyika sambamba na kutoa elimu ya usafi wa Mazingira.
Shabaan amesema anaunga mkono juhudi za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, katika utunzaji nazingira na kuweka mji katika hali ya usafi.

