Barrick Tanzania yatoa ufadhili kwa wanafunzi watano kusoma utaalamu fani ya madini nje ya nchi

Kuendelea kuwekeza kwenye ujuzi, maarifa kwa maendeleo ya sekta ya madini



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Kampuni ya Barrick nchini inayoendesha shughuli zake kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Twiga Minerals imetoa ufadhili kwa wanafunzi watano kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwenda kusoma Shahada ya kwanza ya Elimu ya Madini na Jiolojia katika Chuo Kikuu cha Johannesburg Afrika ya Kusini kupitia progamu yake ya kuwezesha wasomi vijana inayotekelezwa kanda ya Afrika na Mashariki ya kati.

Akizungumza kwenye hafla ya kutangaza ufadhili huo na kuwaaga wanafunzi waliofanikiwa kupata fursa hiyo jijini Dar es Salaam , Meneja wa Barrick nchini, Dkt Melkiory Ngido alisema ufadhili huu ni ushuhuda na uthibitisho kwamba Barrick imelenga kukuza sekta ya madini kupitia uwekezaji wake sambamba na kuhakikisha sekta ya madini inatoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi.

“Uwajibikaji wetu hauishii kuendesha migodi yetu kwa viwango vya kimataifa bali pia tumejikita kuhakikisha tunawekeza katika kuwapatia watanzania ujuzi hususani kwa vijana ambao watakuwa wataalamu wa siku za usoni,ndio maana kupitia udhamini wa elimu kama huu kunawezesha kuwa na wataalamu wa fani ya madini na wabunifu watakaochangia kuleta maendeleo katika siku za usoni”alisema Dkt.Ngido.

Aliongeza kwamba huu ni Ushahidi tosha kwamba kampuni ya Barrick sio tu kwenye uchimbaji wa madini bali pia kwenye uwekezaji wa watu hususani watanzania kwenye elimu , ujuzi , maarifa na teknolojia ili wawe wataalamu na wabobezi kwenye sekta ya madini nchini siku za usoni.

Alisema Barrick itakuwa karibu na Wanafunzi hao na pindi wakapomaliza masomo yao watapatiwa fursa ya kuwajengea uwezo wa kupata ujuzi zaidi kwa kuwapatia ajira katika migodi yake nchini.

“Moja ya majukumu yetu sio tu jinsi tunavyochimba madini bali hasa sisi ni nani kwenye uwekezaji kwa watu na jinsi tunavyotazama siku za usoni kwa viongozi vijana kwa kupitia elimu tunafanya uwekezaji na mipango ya muda mrefu kwenye ujuzi , ubunifu na maendeleo ya taifa,” alifafanua Dkt Ngido

Aliongeza kwamba dhamira ya kampuni ya Barrick ni kuendelea na ushirikiano wenye tija kwa kufanya uwekezaji endelevu wenye tija kwa Tanzania na watu wake kwa kuhakikisha kwamba katika programu hii taifa linaweza kupata wataalamu mbalimbali kwenye fani ya Uinjinia wa madini na Jiolojia hapa nchini.

Pamoja na mambo mengine alifafanua kwamba kupitia programu hiyo kampuni ya Barrick kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wataendelea na kuhakikisha wanazalisha wataalamu wapya kwenye sekta ya madini hapa nchini.

Kwa upande wake , Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa William Anangisye alishukuru kwa kampuni ya Barrick kuwapa ufadhili wanafunzi watano kutoka kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) baada ya kushindanishwa na wenzao kutoka Vyuo vikuu vingine hapa nchini.

“Tumefurahi na ufadhili huu na ni Imani yangu watakwenda kusoma kwa bidhii na hakuna atayerudishwa kwa kushindwa masomo nawataka muwe mabalozi wazuri kwa Chuo chetu na nchini kwa ujumla,” alisema Profesa Anangisye

Alisema kwamba ufadhili huo ni ishara tosha kwamba sekta binafsi na za umma zinaweza kushirikiana sio tu kwenye mambo ya fedha bali pia kwenye uwekezaji wa namna hii kwenye sekta ya elimu wenye maono na manufaa mapana na makubwa kwa maendeleo ya taifa na watu wake.

Alisema ufadhili wa wanafunzi hawa umekuwa baada ya mchujo wa wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali hapa nchini na hatimaye hawa wameshinda , hawa ni kati ya wanafunzi bora waliopita kwenye mchujo na kupata ufadhili kwa kwenda kusoma shahada ya kwanza kwenye madini,” .

“Ni furaha yangu kuona kwamba kati ya wanafunzi hawa waliopata ufadhili kuna wasichana hii ni moja ya sera ya pale mlimani kuweka uwiano wa jinsia kwenye masomo ili kuhakikisha watoto wa kike na wenye uwezo wanapata fursa za kusonga mbele,” alisisitiza

Profesa Anangisye alifafanua kwamba ushirikiano huo kati ya sekta binafsi na za umma ni muhimu kuendelea kudumisha na kupanua wigo wake kwa maslahi ya watanzania katika kuleta msukumo wa maendeleo ya kisekta na uwekezaji kwenye rasiliamali watu.

Mmoja ya wanafunzi akiongea kwa niaba ya wenzake, Samson Abeid alisema kwamba programu hiyo ni fursa ya kipekee kwa wanafunzi wa kitanzania kwa kusoma kwa bidii na kuhakikisha kwamba wanatoa mchango katika maendeleo ya taifa.

“Programu hii itachochea chachu katika sekta ya elimu hapa nchini na kutoa fursa kwa wanafunzi wa kitanzania kupata elimu , maarifa na ujuzi nje ya nchini,” alisema Abeid

Kampuni ya Barrick nchini inaendesha migodi mitatu makubwa , Bulyanhulu , uliopo kahama , Shinyanga , North Mara , Tarime , Mara na Buzwagi ambao upo katika hatua za mwisho za ufugaji uliopo, Kahama. 



Barrick Tanzania yatoa ufadhili kwa wanafunzi watano kusoma utaalamu fani ya madini nje ya nchi Barrick Tanzania yatoa ufadhili kwa wanafunzi watano kusoma utaalamu fani ya madini nje ya nchi Reviewed by Gude Media on 4:09:00 AM Rating: 5

No comments

Note: Only a member of this blog may post a comment.