Balozi wa Canada nchini apongeza uendeshaji wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu na ufanikishaji miradi ya kijamii

Balozi wa Canada nchini, Emily Burns (wa pili kulia), akiangalia shughuli za uzalishaji chini ya mgodi (Underground) kwenye ziara yake ya kikazi katika mgodi wa Barrick Bulyanhulu.  Kulia ni Meneja Mkazi wa Barrick nchini , Dkt Melkiory Ngido na maofisa kutoka ubalozi wa Canada nchini.

Balozi wa Canada nchini Tanzania, Emily Burns, amefanya ziara ya kikazi katika mgodi wa dhahabu wa Barrick Bulyanhulu uliopo katika halmashauri ya wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga na kupongeza uendeshaji wa mgodi huo kwa viwango vya kimataifa sambamba na kufanikiwa kutekeleza malengo Endelevu ya Dunia (SDGs) kwa vitendo.

Burns, katika ziara hiyo alitembelea maeneo ya uzalishaji na kuona jinsi kampuni ya Barrick ilivyowekeza katika matumizi ya teknolojia za kisasa na zenye usalama kwa wafanyakazi katika shughuli za uchimbaji ambapo pia alitembelea baadhi ya miradi ya kijamii iliyotekelezwa kwa fedha za uwajibikaji kwa jamii kutoka mgodi wa Barrick Bulyanhulu ambayo ni kituo cha afya cha Bugarama na shule ya sekondari ya Bugarama.

Akizungumza baada ya ziara hiyo Balozi Burns, ametoa pongezi kwa Kampuni ya Barrick nchini kwa kuendesha migodi yake kwa weledi mkubwa na kuhakikisha uwekezaji wake unaleta manufaa kwa jamii zinazozunguka maeneo ya migodi kupitia utekelezaji wa miradi ya kijamii.

Amesema mgodi huo hutoa mchango wa ukuzaji uchumi wa taifa kwa ujumla kupitia kulipa kodi Serikali na kupanua wigo wa ajira kwa watanzania walioajiriwa migodini na wale wenye ajira zisizo za moja kwa moja ikiwemo wazabuni wanaofanya kazi na migodi.

"Nachukua nafasi hii kuipongeza Kampuni ya Barrick kupitia Mgodi wake wa Barrick Bulyanhulu kwa jinsi unavyoendesha shughuli zake za uzalishaji kwa weledi kwa kuzingatia Usalama kwa Wafanyakazi wake na kwa jinsi unavyoshirikiana na Serikali na Jamii inayozunguka mgodi kwa kuwawezesha miradi ya maendeleo pamoja na vikundi mbalimbali vya wajasiriamali", amesema Balozi Emily Burns.

Naye Meneja Mkazi wa Barrick nchini (Country Manager), Dk.Melkiory Ngido, ametoa shukrani kwa Balozi wa Canada nchini kwa kutembelea mgodi wa Barrick Bulyanhulu na kutembelea baadhi ya miradi ya kijamii Iliyotekelezwa na mgodi huo ambayo imelenga kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi maeneo ya jirani na mgodi na jamii kwa ujumla.

"Kwetu ziara hii ni chachu ya kujifunza na kupokea maoni kutoka kwa wadau ili kuongeza jitihada za kufanya vizuri zaidi”, amesema.

Dk.Ngido ameongeza kusema kuwa dhamira ya Kampuni ya Barrick inayoendesha shughuli zake nchini kwa ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals ni kuunga mkono jitihada za serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na mahitaji muhimu ili kunufaika na uwekezaji wake nchini.

Pia amesema utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii ni mkakati endelevu wa kampuni ya hiyo, unaojumuisha ushirikiano na wadau na vipaumbele ambavyo vimelenga kufanikisha kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii zinazoishi kwenye maeneo yaliyopo jirani na migodi yake na kufanikisha utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Dunia (SDGs).

Balozi wa Canada nchini, Emily Burns, akiangalia mashine ya teknolojia ya kisasa ya uchimbaji madini bila kulazimika kushuka chini ya ardhi alipotembelea mgodi wa Barrick Bulyanhulu.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bugarama, Eveline Kajigiri, akielezea maendeleo ya shule kwa Balozi wa Canada nchini, Emily Burns alipotembelea shule hiyo inayofadhiliwa na mgodi wa Barrick Bulyanhulu, wakati wa ziara ya kutembelea mgodi huo na baadhi ya miradi ya kijamii iliyotekelezwa na mgodi. Kushoto ni Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido na wafanyakazi wa mgodi wa Balyanhulu.