DC Kibaha awataka walimu kuwafahamu wanafunzi kubaini changamoto zao



Na Mwandishi Wetu, KIBAHA


Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon, amewataka walimu na wasimamizi wa shule kufahamu na kuwafuatilia kwa karibu wanafunzi ili kubaini changamoto zao.

Nickson ametoa wito huo, katika uzinduzi wa ugawaji wa madawati, viti na meza kwa shule za msingi na sekondari za Manispaa ya Kibaha, uliofanyika Shule ya Msingi Mkoani, Mkoa wa Pwani.


Amesema uwepo wa miundombinu ya elimu kama madawati, madarasa na walimu pekee hauhakikishi mwanafunzi kujifunza ipasavyo, iwapo changamoto binafsi za mwanafunzi hazitatambuliwa na kushughulikiwa.


“Lazima tuwafahamu wanafunzi, uwepo wa madawati, madarasa na walimu hauimaanishi moja kwa moja kuwa mwanafunzi anajifunza, kujifunza kunategemea na mazingira ya mwanafunzi mwenyewe,”


Amesema kuwa wanafunzi wanatoka katika mazingira tofauti ya kifamilia, hali inayoweza kuathiri mwenendo wao wa masomo.


“Wapo wanafunzi wanaotoka familia kamili za baba na mama, wengine wanaishi na mzazi mmoja, wengine hawana wazazi na wapo chini ya wasimamizi, Wapo wanaotoka familia zenye migogoro, wengine wazazi hawapo salama, wapo wanaolala wamekula na wengine hawajala. Ili tuwasaidie, ni lazima tuwafahamu,” amesema Nickson.


Nickson amesema walimu na wasimamizi wa shule wanapowafahamu mazingira ya mwanafunzi, inakuwa rahisi kutoa msaada unaofaa na kuboresha ufaulu wao.


Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dk. Nicas Mawazo, amesema idadi ya wanafunzi katika manispaa hiyo imeendelea kuongezeka, hali inayoongeza uhitaji wa miundombinu ya elimu.


Amesema kwa shule za sekondari, idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 19,609 mwaka 2025 hadi 22,138 mwaka huu, huku shule za msingi ongezeko ni kutoka wanafunzi 44,128 hadi 46,324 katika kipindi hicho.


Pia Dk. Mawazo amesisitiza kuwa hakuna mwanafunzi atakayekaa chini kwa kukosa dawati, akiwataka wakuu wa shule kusimamia matumizi na utunzaji wa madawati hayo ili yadumu kwa muda mrefu.


Amesema madawati yanapoharibika wasimizi wasiyatelekeze badala yake wayakarabati ili yaendelee kutumika.


Naye Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Dk. Rogers Shemwelekwa, amesema utengenezaji wa madawati hayo ulianza Novemba 12, 2025 na unatarajiwa kukamilika Machi 29 mwaka huu.


Amesema mradi huo wa madawati unatekelezwa kwa kutumia fedha za mapato ya ndani ya Manispaa hiyo,  ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha mazingira na elimu. 







DC Kibaha awataka walimu kuwafahamu wanafunzi kubaini changamoto zao DC Kibaha awataka walimu kuwafahamu wanafunzi kubaini changamoto zao Reviewed by Gude Media on 8:25:00 AM Rating: 5

No comments

Note: Only a member of this blog may post a comment.