Segerea yaitika Bonnah akichukua fomu za uteuzi ubunge


Na MWANDISHI WETU

Wanachama, wapenzi  wa Chama Cha Mapinduzi  (CCM) na wananchi  katika Jimbo la Segerea, wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam, leo  wamejitokeza kumsindikiza Mgombea Ubunge wa  jimbo hilo  Bonnah Kamoli, kuchukua  fomu  ya  uteuzi katika Ofisi za  Tume  Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC)  wilayani humo.


Msafara wa magari, pikipiki na  bajaji wa mgombea huyo  uliopambwa kwa shamrashamra, ngoma, matarumbeta  na nyimbo za  kuisifu  CCM   ulianzia  katika eneo la Tabata Shule, saa 6:00 mchana, kupitia Tabata Segerea, kisha kuingia Barabara ya Segerea-Majumba Sita na kuingia Barabara ya Nyerere kisha  Mtaa wa Lumumba zilipo ofisi ndogo za INEC.


Bonnah, alipanda gari linalofunguka kwa juu na  kujitokeza katika paa la gari hilo  huku akipunga mkono na kupeperusha  bendera  ya CCM katika mitaa msafara huo ulipopita.


Mgombea huyo alikabidhiwa fomu na  Msimamizi wa Uchaguzi   wa INEC katika  majimbo ya Segerea, Kivule, Ukonga na Ilala, Faraja Nakua.